Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Morata, Rodri wapo hatarini suala la ubaguzi

Morata X Rodri Morata, Rodri wapo hatarini suala la ubaguzi

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirikisho la Mpira wa Mguu Ulaya (Uefa) limefungua jalada la uchunguzi juu ya wachezaji wawili wa Hispania, Rodri na Alvaro Morata kutokana na kitendo walichofanya wakati wa sherehe za ubingwa wa Euro 2024 waliochukua na Hispania nchini Ujerumani kwa kuibamiza England mabao 2-1.

Wawili hao walikuwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha Hispania na hata wakaiwezesha kushinda taji hilo la nne katika historia ya mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya soka barani humo.

Katika sherehe za ubingwa huo zilizofanywa katika Jiji la Madrid, Jumatatu, wiki hii, Morata alianzisha wimbo uliokuwa ukiimba hivi: “Ni Hispania, Gibraltar ni Hispania pia”, akimaanisha eneo dogo lililopo kusini mwa Hispania ambalo linamilikiwa na Uingereza kuwa ni mali ya Hispania.

Baada ya Morata kuimba hivyo kiungo wa kati wa Manchester City, Rodri alichukua kipaza sauti na kuendeleza wimbo huo ulioitikiwa pia na mashabiki kibao waliokuwepo.

Wakati Rodri anachukua kipaza sauti na kuimba, Morata alimwambia,”wewe ujue unacheza England.”

Gibraltar ilitambulika rasmi kama eneo linalomilikiwa na Uingereza 1713 na mara kadhaa Hispania ilijaribu kutaka kulifanya kuwa sehemu ya nchi hiyo, lakini imeshindikana.

Baada ya video hiyo kusambaa, Chama cha Soka cha Gibraltar kiliwasilisha malalamiko kwa Uefa mapema wiki hii na baada ya kuwasilisha Uefa imemteua mtu wa kuchunguza na kama kukiwa na kosa hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya nyota hao.

Taarifa kutoka Uefa zilisema: “Mkaguzi wa maadili na nidhamu wa Uefa anateuliwa kutathmini uwezekano wa ukiukaji wa kanuni za nidhamu za Uefa kwa wachezaji wa Hispania, Rodrigo Hernandez Cascante (Rodri) na Alvaro Morata katika tukio walilofanya hadharani Julai 15, jijini Madrid. Taarifa zaidi zitatolewa”

Haijulikani ni aina gani ya adhabu ambayo Morata, Rodri na pengine FA ya Hispania wataipata ikiwa watapatikana na hatia ya kukiuka kanuni za Uefa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live