Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Molinga kuibeba tena Yanga ikiikabili Coastal Union?

78679 Molinga

Mon, 7 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Yanga inaikabili Coastal Union leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku ikitakiwa kushinda ili kushusha presha ya mashabiki wake, lakini wakitaka kuona mchezaji wao, David Molinga iwapo ataendeleza moto wa kufunga mabao.

Yanga ambayo iko nafasi ya pili kutoka mkiani kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi moja imeshacheza michezo miwili na haijapata ushindi. Ilianza kufungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting na kutoka sare ya mabao 3-3 na Polisi.

Leo, macho ya mashabiki wa Jangwani yatakuwa kwa Molinga ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo uliopita na kuiokoa kulala mbele ya Polisi Tanzania, hivyo anabebeshwa mzigo wa kuipa ushindi wa kwanza msimu huu.

Mashabiki wa Yanga bado hawajamuelewa Molinga licha ya kwamba Kocha mkuu, Mwinyi Zahera kumtetea akiwataka wampe muda ili awe fiti kwani atawashangaza na hawataamini.

Hata hivyo, Molinga ambaye ni mrefu na mwenye mwili uliojazia ameanza kuwajibu waliokuwa wakimdhihaki kwa kuona kuwa Yanga imesajili galasa.

Katika mchezo uliofanyika Alhamisi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania mchezaji huyo aliiokoa timu yake kulala baada ya kufunga mabao hayo ndani ya dakika nne.

Pia Soma

Advertisement
Kabla ya mchezaji huyo kufunga alikosa mabao manne akiwa ana kwa ana na kipa wa Polisi Tanzania, Kulwa Manzi ambapo mashabiki waliohudhuria walianza kupiga kelele wakimtaka kocha msaidizi, Noel Mwandila amtoe.

Dakika chache baadaye, Molinga alifunga mabao mawili na kwa kuonyesha kuwa hakujali zoemeazomea ya mashabiki alikimbilia upande walikokuwa na kushangilia pamoja nao.

Mabao matano mechi tatu

Hadi sasa Molinga ameifungia Yanga mabao matano katika mechi tatu zikiwemo mbili za kirafiki na moja ya Ligi Kuu.

Katika mechi na Polisi Tanzania alifunga mabao mawili, lakini akianza kufunga katika michezo wa kirafiki jijini Mwanza dhidi ya Pamba FC Septemba 7 akiisawazishia Yanga bao kwa shuti kali katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Pia Septemba 10 alifunga mabao mawili - moja la kichwa na lingine kwa shuti katika mchezo wa kirafiki walipoifunga Toto Africans mabao 3-0.

Kocha Zahera aliwahi kukaririwa akisema Molinga alichelewa kujiunga na kikosi hivyo anatakiwa kupewa muda na kudai kuwa, kama asipofunga mabao 15 hadi 20 msimu huu, basi kocha huyo akatwe mkono au awape Dola 1,000 wasioamini maneno yake.

Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema matokeo yasiyoridhisha ya Yanga katika michezo ya karibuni yataufanya mchezo huo kuwa mgumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz