Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Molinga akoleza moto wa mabao

95056 Molinga+pic Molinga akoleza moto wa mabao

Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nyota ya David Molinga imeendelea kung’ara baada ya jana kufunga bao pekee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Yanga ilishinda dhidi ya Ruvu Shooting.

Molinga raia wa DR Congo, alifunga bao hilo dakika 39 kwa mpira wa kichwa akiunganisha krosi ya Ditram Nchimbi aliyopiga upande wa kulia. Mshambuliaji huyo alijiweka katika mazingira mazuri ya kufunga baada ya kuwazidi mbinu mabeki wawili wa Ruvu Shooting ndani ya eneo la hatari. Yanga ilishinda bao 1-0.

Molinga ambaye alitoka kipindi cha pili na kuingia Gnamien Yikpe katika mchezo wa jana, amefikisha mabao saba msimu huu.

Mabeki Santos Mazengo na Baraka Mtui, walichuana na Molinga ambaye dakika 20 alikosa bao la mpira wa kichwa kufuatia krosi ya Juma Abdul.

Pia dakika ya 25 alishindwa kufunga baada ya kiki yake kutua mikononi mwa kipa wa Ruvu Shooting Mohammed Makaka.

Mabeki wa Yanga Lamine Moro na Ally Mtoni walikuwa na kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao ambao walikamata idara ya kiungo.

Pia Soma

Advertisement
Kiungo wa zamani wa Simba, Shabani Kisiga alimiliki sehemu kubwa ya eneo hilo hatua iliyowapa wakati mgumu mabeki wa Yanga na kipa Metacha Mnata.

Baada ya kusajili wachezaji sita katika dirisha dogo na kuboresha benchi la ufundi kwa kumpata kocha Luc Eymael, Yanga ilikuwa na deni la kulipa kisasi dhidi ya Shooting.

Akizungumza jana, Eymael alisema Yanga ilikuwa na nafasi nzuri ya kufunga idadi kubwa ya mabao, lakini kipa wa Ruvu Shooting alikuwa kikwazo.

“Nampongeza kipa wa wapinzani wetu, alicheza kwa ustadi na alikuwa kikwazo kwetu kupata mabao, aliokoa michomo mingi ya wachezaji wangu. Nawapongeza kwa kazi nzuri,”alisema Eymael raia wa Ubelgiji.

Kocha wa Ruvu Shooting Salum Mayanga alisema timu yake ilicheza kwa kiwango bora, lakini kosa moja lilitoa nafasi kwa Yanga kupata bao hilo. Mchezo wa Agosti 28, 2019 Yanga ilifungwa bao 1-0 kwenye uwanja huo.

Hii itakuwa mechi ya nne Yanga kupata ushindi mfululizo baada ya kuzicharaza Singida United, Mtibwa Sugar na Lipuli.

Katika mchezo huo mwamuzi Rafael Ikambi wa Morogoro alilalamikiwa na Yanga baada ya Benard Morrison kufanyiwa faulo na beki wa Ruvu Shooting ndani ya eneo la hatari, badala yake aliamuru ipigwe kona.

Tukio hilo limekuja wakati kukiwa na malalamiko ya waamuzi kudaiwa kushindwa kutafsiri sheria katika mechi za Ligi Kuu Bara hivi karibuni

Ruvu Shooting: Mohammed Makaka, Omari Kindamba, Kassim Simbaulanga, Santos Mazengo, Baraka Mtuwi, Zuberi Dabi, William Patrick, Shabani Kisiga, Fully Maganga, Graham Naftal na Abdallahman Mussa.

Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Ally Mtoni, Papy Tshishimbi, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, David Molinga, Mapinduzi Balama na Bernard Morrison.

Chanzo: mwananchi.co.tz