Wakati baadhi ya klabu za Ligi Kuu zikihaha kutafuta makocha wakuu na wasaidizi, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed ‘Bares’, amesema yupo tayari kuifundisha timu yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara kama atafuatwa na kuelewana maslahi.
Bares aliyeitoa Prisons mkiani na kufanya kuwa timu tishio kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, amesema hahitaji kujipigia debe sana kwani watu wote kazi yake wameiona, hivyo yupo tayari kufanya kazi na klabu yoyote.
“Ligi imemalizika, mwenye kuona kazi ya Bares ameiona kama anahitaji mazungumzo mimi niko tayari, watu wa mpira sisi tunaangalia zaidi maslahi na si kitu kingine, pamoja na kwamba bado ni kocha wa Prisons, lakini wapo watu wanaweza kunipa maslahi mazuri zaidi ya haya ninayoyapata, haya ndiyo maisha ya wacheza soka na makocha, milango iko wazi,” amesema Bares
Akiwazungumzia pia mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, timu yake ya zamani ya Mlandege, amesema ni kati ya jambo ambalo atabaki analikumbuka hasa kwa uamuzi wake kuacha kuinoa timu ambayo ilikuwa bingwa na mshindi wa pili wa Ligi Kuu Zanzibar, na kwenda kuinoa Prisons iliyokuwa inashika nafasi ya mwisho kwenye Ligi Kuu Bara.
Tujipongeze Prisons kwa sababu tumetoka kwenye nafasi mbaya sana, kuna wakati tulikuwa mkiani, tukapanda, inafika wakati mechi za kumalizia ligi hatukuwa miongozi hata mwa timu zilizo kwenye hatari ya kucheza ‘play off”, na umekuwa msimu ambao nimeweka kumbukumbu ambayo sitoisahau kwenye soka la Tanzania tangu nilipoanza kufundisha mpira wa miguu, nililchukua timu kwenye wakati mgumu, ilikuwa ni kama nimejivisha mwenyewe mabomu.” amesema