Nyota ya nahodha wa timu ya Taifa Tanzania na klabu ya KRC Genk, Mbwana Samatta inapitia kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kutamba hadi sasa kwenye kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji, huku straika wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogela akifungukia kinachomsibu.
Msimu wa 2018-2019, Samatta alijitengenezea ufalme KRC Genk na Ligi Kuu nchini humo alipofunga mabao 20 na matatu katika mchujo kuwania ubingwa na kumfanya amalize na mabao 23 ya ligi huku kwenye mashindano yote akimaliza na mabao 32 katika mechi 51 alizocheza.
Msimu wa 2018-2019 alicheza mechi 20 na kufunga mabao saba, kisha 2019-2020 akasajiliwa Aston Villa kwenye Ligi Kuu England alikocheza mechi 14 za ligi na kufunga bao moja huku kwenye Kombe la Carabao alicheza mechi mbili na kufunga bao moja.
Baada ya hapo alitolewa kwa mkopo 2020-2021 kwenda Uturuki katika Klabu ya Fenerbahce na alicheza mechi 30 kwenye mashindano yote.
Akiwa na timu hiyo kwenye Ligi Kuu alicheza mechi 27 na kufunga mabao matano na kwenye Kombe la FA nchini humo alicheza mechi tatu na kufunga bao moja.
Msimu wa 2021-2022, Fernabahce ilimnunua na kumtoa kwa mkopo Royal Antwerp ya nchini Ubelgiji na alicheza mechi 27 za Ligi Kuu nchini humo na kufunga mabao matano tu na kutoa pasi nne za mabao huku upande wa Europa League akicheza mechi sita na kufunga mabao matatu.
Samatta msimu huu yupo kwenye kikosi cha KRC Genk kwa mkopo hali imezidi kuwa mbaya kwake kwani kwenye mechi 16 amefunga bao moja tu akiwa ametumia takribani dakika 385 na kumpa fursa nyota wa Nigeria, Paul Onuachu ambaye ni kinara wa mabao kwenye ligi akiwa na Genk akifunga 16 katika mechi 19, alizocheza hadi sasa.
WADAU WAFUNGUKA
Mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema Samatta ni mchezaji mkubwa na ni sehemu ndogo ambayo atakuwa amekwama tu lakini sio kwamba kiwango chake kimeshuka.
Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema jambo ambalo limemfanya Samatta awe kwenye wakati mgumu kufunga kwa sasa ni kama ilivyokuwa zamani kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamkabili.