Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Modric amaliza ufalme wa Messi Ballon d'Or

30024 Pic+modric Kiungo mahiri wa Croatia na Real Madrid, Luka Modric

Tue, 4 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Paris, Ufaransa. Kiungo mahiri wa Croatia na Real Madrid, Luka Modric, (33), ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2018 ‘Ballon d'Or’, akimaliza ufalme wa muongo mmoja wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Modric alikuwa na mwaka mzuri, Mei mwaka huu alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Real Madrid, kabla ya kuifikisha Croatia katika fainali ya Kombe la Dunia 2018 ikiwa ni mara ya kwanza kwa Taifa hilo kufika hatua hiyo. Pia aliteuliwa mchezaji bora wa fainali hizo za 31 zilizofanyika Russia.

Kiungo huyo amemaliza ufalme waliokuwa nao Ronaldo na Messi ambao walipokezana tuzo hiyo kwa miaka kumi mfululizo kila mmoja akitwaa mara tano.

Katika tuzo hizo zinazotolewa na jarida maarufu la michezo la Ufaransa, mshindi wa pili ni Ronaldo, aliyejiunga na Juventus Julai, mwaka hu.

Nafasi ya tatu imetwaliwa na mshambuliaji wa Atletico Madrid na Ufaransa, Antoine Griezmann, nafasi ya nne Kylian Mbappe wa PSG na Ufaransa na tano bora inakamilishwa na Messi.

Mwafrika pekee aliyekuwa akiwania tuzo hiyo ni nahodha wa Misri na mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye alishika nafasi ya sita.

Nafasi ya saba ilitwaliwa wa Real Madrid na Ufaransa, Raphael Varane akifuatiwa na kiungo wa Chelsea na Ubelgiji, Eden Hazard nafasi ya tisa kiungo wa Manchester City na Ubelgiji, Kevin de Bruyne na kumi bora ilihitimishwa na nahodha wa England na mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane.

Mwafrika pekee aliyewahi kutwaa tuzo hiyo ni Rais wa Liberia, George Weah aliyetwaa mwaka 1995 ambapo pia alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika na Ulaya.

Tuzo za Ballon d'Or zilianzishwa mwaka 1956 na gazeti la michezo Ufaransa na mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo alikuwa staa wa Blackpool na timu ya Taifa ya England, Stanley Matthews.

Katika zama hizo, Matthews alikuwa mchezaji mahiri aliyeitumikia England katika michezo 54 akifunga mabao 11 kuanzia mwaka 1934 hadi 1957 alipostaafu soka.

Kabla ya mwaka 1995, tuzo hizo zilikuwa zinatolewa kwa wachezaji wazawa wa Ulaya lakini kuanzia hapo zilianza kutolewa kwa mchezaji yeyote anayecheza Ulaya.

Kati ya mwaka 2010 hadi 2015 tuzo hizo zilisimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), baada ya kufanya makubaliano na gazeti lililokuwa likiendesha tuzo hiyo lakini kufika 2016, Fifa ilijitoa na kurejesha kwa waasisi.

Washindi wa tuzo hizo kuanzia 2008 – 2017 Ballon d'Or ilitwaliwa na Ronaldo na Messi waliokuwa wakibadilisha kutegemeanza zaidi na mafanikio waliyopata katika klabu zao.

Mwaka          Mshindi                    Mshindi wa pili                  Mshindi wa tatu

2007              Kaka                           Cris Ronaldo            Lionel Messi

2008              Cris Ronaldo Lionel Messi             Fernando Torres

2009              Lionel Messi Cris Ronaldo            Xavi

2010              Lionel Messi Andres Iniesta                     Xavi

2011              Lionel Messi Cris Ronaldo            Xavi

2012              Lionel Messi Cris Ronaldo             Andres Iniesta

2013              Cris Ronaldo Lionel Messi             Franck Ribery

2014              Cris Ronaldo Lionel Messi             Manuel Neuer

2015              Lionel Messi Cris Ronaldo            Neymar

2016              Cris Ronaldo Lionel Messi             Antoine Griezmann

2017              Cris Ronaldo Lionel Messi             Neymar

2018              Luka Modric             Cris Ronaldo            Antoine Griezmann



Chanzo: mwananchi.co.tz