Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moallin alianika bao la Msomalia

Moallin Moallin alianika bao la Msomalia

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya KMC, kushinda bao 1-0 dhidi ya Ihefu, kocha mkuu wa timu hiyo, Abdihamid Moallin amesema aliota nyota mpya wa kikosi hicho Msomalia, Ibrahim Elias atafunga ndio maana akamuingiza haraka kipindi cha pili.

Nyota huyo aliyesajiliwa msimu huu na KMC akitokea klabu ya Kibra United ya nchini Kenya alifunga bao hilo la ushindi ikiwa ni muda mchache tu tangu aingie kipindi cha pili akichukua nafasi ya Darueshi Saliboko.

Akizungumza nasi jijini Dar es Salaam, Moallin alisema awali mchezaji huyo alikuwa kwenye mipango ya kuanza kikosi cha kwanza ila aliona anaweza kuisaidia timu hiyo pindi tu mambo yatakapokuwa magumu kwao.

“Alifanya kile ambacho tulimuagiza kwa sababu ukiangalia kwa jinsi ambavyo mchezo ulikuwa unaendelea ni wazi kulikuwa na makosa ambayo wenzetu walikuwa wanayafanya hivyo tukamuelekeza na akayafanyia kazi,” alisema.

Moallin aliongeza sababu kubwa ya kutompa nafasi ya kucheza mara kwa mara ni kutokana na kumpunguzia presha kwa sababu anahitaji kuzoea soka la Bongo kidogo kidogo kwani mazingira ya alikotoka na huku yana utofauti.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa KMC baada ya kuifunga JKT Tanzania na Geita Gold mabao 2-1 kila moja na kuifanya ifikishe pointi 10 na kujisogeza kutoka nafasi ya tano hadi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live