Kocha wa Azam FC, Abdihamid Moallin ameanza mikwara mapema akitamba, pointi tatu walizozipata dhidi ya Namungo, zimeongeza chachu ya ushindani kuelekea mchezo wao na Yanga Aprili 6 mwaka huu.
Azam ndio timu ya mwisho kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara ilipofanya hivyo Aprili 25 mwaka jana kwa bao la Prince Dube, ambaye juzi alirejea kwa kishindo katika kilosi hicho kwa kufunga bao la kwanza dhidi ya Namungo katika mechi iliyopigwa katikati ya wiki mjini Lindi na kufuta gundu la timu hiyo kucheza mechi tatu mfululizo bila ushindi wala kufunga bao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Moallin alisema ushindi huo wa 2-0 ugenini umerudisha morali kwa mastaa wake kuelekea mchezo wao na Yanga ambao anaamini utakuwa mgumu kutokana na kukutana na timu ambayo ina mwendelezo wa matokeo mazuri.
“Hatukuwa na matokeo mazuri kwenye michezo mitatu mfululizo timu ilikuwa inacheza kwa presha jui imetulia imetanguliwa bao dakika za mapema lakini ikaonyesha ukomavu kwa kusawazisha na kufunga bao la ushindi,” alisema.
Moallin alisema anajua kama Ligi ya Bara ni ngumu lakini kinachompa matumaini ni uimara wa wachezaji wake ambao wameonekana kuwa fiti huku akiweka wazi kuwa anatarajia kutumia muda uliopo kukiandaa zaidi kikosi chake.
Alisema kuwa kila siku amekuwa akikifanyia marekebisho kikosi chake mazoezini kwa kuwafundisha wachezaji wake mbinu mbalimbali pamoja na mifumo ya kisasa ambayo inaweza kuwapa matokeo mazuri na anafurahi kuona hilo linafanyiwa kazi ipasavyo na ndiyo maana wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye mechi za ligi.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28 baada ya kucheza michezo 18 ikishinda nane, sare nne na kupoteza michezo sita.