Gwiji wa soka wa Misri, Ahmed Hossam 'Mido' amemuweka kwenye kiti cha moto tena Mohamed Salah baada ya majeraha kumlazimisha staa huyo kurejea Liverpool kutoka kwenye fainali za Mataifa ya Afrika.
Straika huyo wa Majogoo wa Anfield aliumia wakati akiiwakilisha nchi yake dhidi ya Ghana – jambo lililomlazimisha Salah, 31, kutoka nje kabla ya mechi kumalizika akilalamikia kuumia misuli ya nyuma ya paja. Tatizo hilo limeonekana ni kubwa kuliko lilivyofikiriwa awali, hivyo uamuzi ukachukuliwa kwamba Salah aende akapatiwe matibabu nchini England.
Maswali yamekuwa yakiulizwa kwanini Salah aliamua kuondoka katika kambi ya Misri, wakati angeweza kujifua arejeshe fitinesi yake akiwa kulekule Ivory Coast na kujaribu kujiweka katika nafasi ya kuweza kuendelea kuipigania nchi yake, lakini Jurgen Klopp amedai kuwa supastaa huyo atapata "matibabu sahihi" Anfield.
ALICHOKISEMA MIDO Mido, ambaye enzi zake anapiga soka alikuwa fundi kwelikweli na aliitumikia klabu ya Tottenham na Middlesbrough kwenye Ligi Kuu England, hajafurahishwa na kauli hiyo ya Klopp.
Baada ya kuona Salah akiposti picha zake akifanya mazoezi mepesi katika uwanja wa mazoezi wa Liverpool, straika huyo wa zamani alisema katika posti yake aliyoiweka katika mtandao wa kijamii: “Oh, mazoezi haya ni machafu na mazito sana, ni magumu kuyafanya isipokuwa ukiwa Liverpool tu.”
KITUO KIFUATACHO KWA MISRI Misri inajiandaa kuikabili DR Congo katika mechi ya 16-Bora ya Afcon Jumapili. Liverpool wamesema Salah atakuwa huru kurejea kujiunga na Mafarao wenzake kama Misri itafika fainali na nahodha wao huyo akathibitisha kuwa amepona tatizo lake.