Arsenal ilishusha pumzi kidogo baada ya Jumapili iliyopita straika Erling Haaland kuumia kwenye mchezo wa Aston Villa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiamini kwamba hatakuwamo uwanjani katika kipute chao cha Emirates usiku wa leo Jumatano.
Lakini, kwa bahati mbaya, straika huyo ambaye amefunga mabao 25 kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, yupo fiti na amefanya mazoezi na wenzake wa Manchester City jioni ya juzi Jumatatu - hivyo atakuwapo uwanjani Emirates.
Straika huyo kiboko ya makipa kwenye Ligi Kuu England alitolewa wakati wa mapumziko kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-1 baada ya kuumia mguu. Baada ya mechi hiyo, kocha Pep Guardiola alisema atalazimika kusubiri hadi kufikia siku ya jana Jumanne ili kujua kama mshambuliaji wake huyo aliyemsajiliwa Pauni 51.4 milioni kutoka Borussia Dortmund mwaka jana atakuwa fiti kwenye kuwakabili vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal huko kwao Emirates.
Lakini, sasa dalili zimekuwa njema, ambapo Haaland, aliyefunga mabao 31 kwenye michuano yote msimu huu, amerudi na yupo fiti. Alifanya mazoezi na wenzake Jumatatu jioni na jana Jumanne alitarajia kujiweka fiti zaidi kwa ajili ya kwenda kuwakabili Arsenal, ambao amewapania kwelikweli. Haaland aliwahi kuwaonya Arsenal akiwaambia kwamba ni wao Man City ndiyo watakaowafunga na kuwaondoa kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.
Hata hivyo, supastaa huyo wa Norway hajafunga bao kwenye mechi tatu zilizopita, huku bao lake la mwisho kufunga ugenini ilikuwa Desemba 28 walipokipiga na Leeds United huko Elland Road. Hakutaka kupiga penalti dhidi ya Aston Villa na kumwaachia Riyad Mahrez afunge, huku akihusika kutengeneza bao la kiungo Ilkay Gundogan.
Lakini, Guardiola alisema Haaland atamtumia kama tu atakuwa fiti kwa asilimia 100, akisema: "Kama hatakuwa tayari, tutachukua tahadhali ya kutomchezesha." Kama Haaland atakosa mechi hiyo, basi Guardiola ataanza na Muargentina, Julian Alvarez - huku Jack Grealish na Mahrez wakitarajia kucheza kwenye wingi. Ushindi utawafanya Man City kuwaengua Arsenal kileleni, lakini chama hilo la Mikel Arteta litakuwa na mchezo mmoja mkononi.