Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mmoja Yanga kumpisha Kisinda, aikataa ofa ya Simba

Tuisila Kisinda Mmoja Yanga kumpisha Kisinda

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dirisha la usajili wa wachezaji nchini limefungwa usiku wa kuamkia leo, lakini habari kubwa huenda ni sapraizi kwa mashabiki wa Yanga ile ya winga teleza, Tuisila Kisinda kuamua kurejea tena Jangwani, lakini aking’oa mtu katika kikosi cha sasa cha Kocha Nasreddine Nabi.

Ndio! Yanga imemrejesha Kisinda ili kuja kuchukua nafasi ya mshambuliaji mmoja kati ya Lazarous Kambole au Heritier Makambo ambaye hadi jana mchana walikuwa wakipigiwa ana ana..ana doo!

Taarifa kutoka Morocco ulipoanzia usajili huo ni kwamba Kisinda ameingia katika mgogoro na klabu ya RS Berkane anayoidai fedha za usajili, huku ikionekana kama anatengwa.

Kisinda anaona ana nafasi ya kuichezea Berkane, lakini shida inakuja mabosi wamekuwa wakishinikiza wachezaji wazawa wapewe nafasi.

Berkane imekanusha madai hayo na kumuambia shida ni kiwango chake na kama anaona ana uwezo atafute timu ya mkopo na wapo wapo tayari kumuachia na jamaa fasta akawasiliana na matajiri wake wa zamani Yanga na mipango ikasukwa mapema kabla dirisha halijafungwa jana usiku.

Hata hivyo taarifa za uhakika zinadai kwamba uongozi wa Kisinda haukutaka chaguo la mkopo ukiwataka Berkane kuvunja mkataba na kumlipa fedha zake. Wakati majadiliano yakiendelea haraka taarifa zikawafikia vigogo Simba na Yanga ambao kila mmoja akitaka saini ya winga huyo ambaye aliwahi kumpa shida beki Joash Onyango.

Habari zaidi zinasema Kisinda aliwagomea Berkane kuzungumza na Simba, kisha akawaambia wazungumze na Yanga ambao Mwanaspoti linafahamu Hersi Said alikuwa kazini akipigania saini hiyo. Kisinda anaamini maisha yake Yanga hayatakuwa magumu endapo akirejea kutokana na jinsi ya kuwafurahisha mashabiki wa Yanga huku pia akivutiwa na uwepo wa Wakongomani wenzake bora hasa mshambuliaji Fiston Mayele.

Yanga pia kupitia Hersi imekuwa rahisi kumshawishi winga huyo aliyepewa jina la TK Master kutokana na kuwa na mawasiliano ya karibu na mapema akamtonya juu ya dili hilo. Berkane tayari imeshakubaliana na Yanga ambao awali walifanya hiyo jana kikao kizito nani aachwe kati ya Kambole au Makambo.

Uamuzi huo waliachiwa makocha Nasreddine Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze waufanye huku Makambo akiwa katika nafasi ngumu kusalia katika timu hiyo.

Awali, hesabu zilikuwa zikimvizia winga Jesus Moloko, lakini ubora wake tangu ligi ianze kila bosi aliingia na wasiwasi na karata kusalia kwa washambuliaji hao wawili.

Tayari mpaka kufikia jana Yanga ilikuwa ikipambana kuingiza jina la Kisinda kwenye usajili mtandaoni (Transfer Matching System, TMS) huku mabosi wakisubiri uamuzi wa makocha. Mapema kocha Nabi alikuwa anahitaji winga mwenye kasi aongezwe katika kikosi akiwapigia hesabu wapinzani wao Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga itaanza raundi ya awali dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini ilioomba kuchezea mechi ya nyumbani Uwanja wa Mkapa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz