Mmiliki wa klabu ya Tottenham Hotspur, Joe Lewis amemtaka Mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy kumpiga bei mshambuliaji Harry Kane ikiwa nyota huyo raia wa England hatasaini nyongeza ya mkataba mpya klabuni hapo.
Vyanzo vimebainisha kuwa Lewis hayuko tayari kumwacha Kane amalize kandarasi yake na kuondoka kama mchezaji huru msimu ujao wa joto hivyo amemtaka Levy kumuuza huku Spurs ikitaka kiasi kisichopungua pauni milioni 100 kumwachia.
Baada ya kushuhudia ofa mbili zikitupiliwa mbali, klabu ya Bayern Munich inaandaa ofa ya tatu kwa ajili ya kumsajili Kane. Spurs ipo tayari kumpatia Kane mshahara wa pauni laki nne (takribani Tsh bilioni 1.26) kwa wiki ili kumshawishi kusalia klabuni hapo.