Kocha wa Bayern Munich, Vincent Kompany amesema kwamba watu wamekuwa wakilitamka jina lake vibaya kwa miaka yote aliyokuwa akicheza soka.
Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 38, aliulizwa usahihi wa jina lake linavyopaswa kutamkwa wakati alipotambulishwa kuwa kocha mpya wa Bayern Munich wiki iliyopita.
Kocha huyo wa zamani wa Burnley alisema jina lake la kwanza linapaswa kutamkwa “Van-sont” huku herufi “t” ikitamkwa kwa kulegeza ulimi.
Lakini, alibainisha kwamba kwa nyakati zake alizocheza soka Ujerumani alipokuwa kwenye klabu ya Hamburg ndipo ilipoanza kukosewa matamshi ya jina lake la kwanza, alipoanza kuitwa “Vincent” au “Vinny” kama Waingereza ambavyo wamekuwa wakilitamka jina hilo.
Kompany alisema: “Hivyo, jina langu linapaswa kutamkwa ‘Van-sont’. Lakini nilipocheza Hamburg kwa miaka mwingi, Wajerumani wakaanza kukosea, na kunitamka ‘Vincent’ au ‘Vinny’.”
Kompany aliitumikia Hamburg kuanzia mwaka 2006 hadi 2008 kabla ya kujiunga na Manchester City, ambako alicheza kwa miaka 11, akichaguliwa nahodha wa kikosi hicho cha Etihad.
Alishinda mataji manne ya Ligi Kuu England, mawili ya Kombe la FA na manne ya Kombe la Ligi.
Aliondoka kwenda kujiunga na Anderlecht mwaka 2019, ambako baadaye alikuwa kocha wao. Alipoondoka kwenye timu hiyo mwaka 2022, alitua Burnley, akawapandisha Ligi Kuu England kabla ya kuwashusha msimu uliopita wa 2023-24. Na sasa amepata kazi Bayern Munich hadi 2027.