Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mmachinga azibeba Simba, Yanga ugenini

Simba Yanga WA0007 Mmachinga azibeba Simba, Yanga ugenini

Mon, 1 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya matokeo yasiyotarajiwa iliyopata Simba na Yanga katika mechi za nyumbani za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns, nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ amezibeba timu hizo zikienda ugenini.

Mmachinga ni mmoja ya wakongwe waliotoa maoni yao juu ya timu hizo juu ya kitu cha kufanya katika mechizo za ugenini zitakazopigwa Ijumaa hii, kwa kuamini zote zina nafasi ya kusonga mbele licha ya kutoshinda nyumbani mbele ya wapinzani wao.

Mmachinga aliyewahi kuwika na timu hizo, akiwa anashikikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika msimu mmoja, alisema anaona nafasi za timu hizo kupata ushindi ugenini, kutokana na aina ya matokeo yaliyopatikana Kwa Mkapa, Simba ikifungwa 1-0 na Al Ahly na Yanga kutoka suluhu na Mamelodi.

“Simba ikacheze kama vile haina cha kupoteza, hilo litaipa Al Ahly presha, pia ijue wapinzani wao hao ni mzuri dakika zipi na zipi inaweza ikatumia kufunga, huku kila mchezaji akatimize majukumu yake bila kujisahau na kumfanya mwingine kuwa na mzigo mkubwa wa majukumu, naamini kabisa inaweza ikashinda ugenini,”alisema Mmachinga aliezichezea pia Bandari, Mbanga, Twiga Sports na Taifa Stars.

“Kwa upande wa Yanga, ikapambane kutangulia kufunga bao, hilo linaweza likaitoa Mamelodi mchezoni, kubwa zaidi ni mbinu za kocha Gamondi kukipanga kikosi chake cha kumpa matokeo,” aliongeza Mmachinga, huku nyota mwingine wa zamani wa Yanga, Kipanya Malapa akaongezea; “Nimetazama Al Ahly na Mamelodi Sandown zinavyocheza zinatumia mbinu kali,lakini zinafungika, kama utulivu ungekuwepo kwa washambuliaji wa Simba na Yanga wangepata matokeo, kwa sababu walipata nafasi za kufunga.”

Kipanya alisema; “Mastaa wa Simba na Yanga nje na mbinu za makocha wanatakiwa wahamasishane na kuweka dhamira ya uzalendo wa kwenda kuzipambania timu hizo, wakifanya hivyo nina uhakika wataweka heshima ugenini.”

Beki mwingine wa zamani wa Simba na Nyota Nyekundu, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema; “Soka linabadilika, Simba na Yanga zinaweza zikawa tishio ugenini zikacheze kama vile hazitacheza tena, hilo litazipa presha timu pinzani kufanya makosa, jambo la msingi wachezaji ni kujitoa.”

Nahodha wa zamani wa Simba aliye kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa alisema timu hizo zinapaswa kwenda kucheza kwa akili zaidi ugenini, kwa kurejea mechi za nyumbani kujua wapi walikosea na wapi na kubaini hatari ya timu pinzani, kisha kujipanga upya akiamini zitafuzu.

Chanzo: Mwanaspoti