Mshambuliaji wa zamani wa Klabu ya Young Africans, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, ameipa mbinu timu hiyo kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Young Africans itaanzia nyumbani Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa keshokutwa Jumatano (Mei 10) kuikaribisha Marumo Gallants, kabla ya kwenye Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Mei 17.
Mmachinga amewataka wachezaji wa Young Africans kucheza kwa umakini na kuhakikisha wanapata mabao mengi katika mchezo Mkondo wa Kwanza, ambao umepangwa kuanza saa kumi jioni kwa saa za Tanzania.
Mmachinga ambaye pia ni Kocha amesema ni vema viongozi, wachezaji na wadau wa timu hiyo wakawa makini kusaka ushindi mkubwa katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza kabla ya kwenda Afrika Kusini ambako anaamni mazingira yatakuwa magumu ndani na nje ya Uwanja.
“Kikubwa katika mechi hii ya kwa sababu wanaanzia kwanza nyumbani ni kuhakikisha wanakuwa makini na mabao kufunga yatakayowaweka mengi katika mazingira mazuri katika mechi ya marudiano,” amesema.
Mmachinga aliwataka wachezaji kujituma uwanjani na kuwahimiza mashabiki kufika kwa wingi kuwapa sapoti wachezaji wa timu hiyo inayowakilisha nchi.