Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlandege walia hujuma kichapo 5-0

Mlandege RXE.jpeg Mlandege walia hujuma kichapo 5-0

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Mlandege FC imeilalamikia Bodi ya Ligi Zanzibar iliyoitaka icheze dhidi ya KVZ licha ya kuiandikia barua ikitaka mchezo usogezwe mbele kufuatia wachezaji kuumwa na ugonjwa wa macho mekundu (red eyes) na hivyo bodi ya ligi kuilazimisha icheze siku hiyo iliyopanga.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Zanzibar uliochezwa Febuari 4 kwenye Uwanja wa Mao Zedong A na Mlandege FC kupokea kichapo  cha mabao 5-0 kutoka kwa KVZ, uongozi kupitia idara ya habari na mawasiliano umelalamika kwa kutoa taarifa ukidai kwamba hawakutendewa haki na kwamba walihujumiwa.

"Uongozi wa klabu ya Mlandege umesikitishwa na kufadhaishwa na uamuzi wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira Zanzibar wa kuamua mchezo wetu dhidi ya KVZ kuchezwa kama ulivyopangwa licha ya kuwaandikia barua ya kuomba usogezwe mbele kutokana na changamoto ya kiafya ya wachezaji wetu," imesema taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Taarifa ya timu hiyo imeeleza kwamba siku mbili kabla ya mchezo huo waliwasilisha barua kwa Bodi ya Ligi kuomba mchezo huo upelekwe mbele kutokana na wachezaji tisa kusumbuliwa na ugonjwa na macho.

"Wakati tunasubiri majibu rasmi ya maandishi kutoka bodi ya kupangiwa tarehe nyingine, tukapokea barua saa tano asubuhi siku hiyo ya mchezo kwamba ombi letu limekataliwa na hivyo mechi itachezwa kama ilivyopangwa," taarifa imeongeza.

Taarifa hiyo imesema kitendo hicho cha kujibiwa saa chache kabla ya mchezo huku wakiwa wamewasilisha barua saa 72 kabla, na wakiwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wanakabiliwa na 'red eyes' wanakitafsiri kama hujuma ya wazi dhidi yao.

Mwanaspoti imewatafuta Bodi ya Ligi ambao ni walalamikiwa na kupitia mtendaji mkuu, Issa Kassim imesema walipokea barua Ijumaa iliyopita saa 8:30 mchana kutoka Mlandege na kwamba ilikuwa ni siku mbili na sio saa 72 kama inavyolalamikiwa na klabu hiyo.

Amesema kikanuni mechi huwa na kikao cha maandalizi (pre match meeting) siku moja kabla ya mchezo na viongozi wa Mlandege walishiriki wakiamini kwamba mchezo uliokuwapo.

"Sisi tuliwajibu muda huo kwa sababu tulifuata utaratibu wa barua walituletea kimaandishi na tukawajibu kimaandishi, lakini tayari wao walishakuja kwenye kikao cha matayarisho ya mechi kwa kuwa wamekubali kucheza," amesema Issa na Kuongeza:

"Na siku hiyo tuliwaambia kuwa pamoja na kupokea ombi lenu mechi ipo kama kutakuwa na lolote tutawajulisha na hiyo siyo hujuma kwa sababu tulifuata kanuni zote za mchezo."

Baadhi ya wadau wa soka wamezungumzia mchezo na sakata hilo wakisema huenda Mlandege kupoteza mchezo huo ndiko kumeibua malalamiko hayo.

Fatawi Ramadhan amesema timu ina wachezaji wengi, hivyo kuumwa kwa mastaa tisa haimaanishi mchezo usichezwe kwa sababu  wengine wapo ambao wanaweza kucheza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live