Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlandege: Tunawajua vizuri Singida BS, hawatutishi

Singida To Final.jpeg Singida Big Stars

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kutinga fainali, Kocha mkuu wa Mlandege, Abdalah Mohamed ‘Bares’ amesema anatambua ubora wa wapinzani wake kwenye hatua hiyo na anajiandaa kupambana nao vyema.

Mlandege imetinga fainali baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo dhidi ya Namungo, hivyo mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penati na kushinda 5-4.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Amaan, Bares alisema amewafuatilia wapinzani wake kwenye mechi zao zote na amebaini ni wazuri maeneo yote lakini wanatumia mipira ya pembeni kushambulia.

“Singida Big Stars ni timu iliyokamilika kila eneo lakini hilo halitutishi, sisi pia ni wazuri na tutajiandaa kwa ajili ya kucheza fainali ambayo tunatarajia itakuwa ya ushindani kutokana na wote kuhitaji taji hili,” alisema na kuongeza;

“Wachezaji wangu wapo imara na wana ari nzuri ya ushindani, nawaamini kutokana na kufuata kile ninachowaelekeza mazoezini hiyo ndiyo siri kubwa ya kufanya vizuri kwenye kila mchezo.”

Alisema anawaheshimu wapinzani wake wapo vizuri na ni washindani wazuri ndiyo maana wamefika hatua hiyo ambayo na wao wameifikia lengo lao sasa ni kuhakikisha taji linabaki Zanzibar baada ya muda mrefu kushindwa kufanya hivyo.

Bares alitumia nafasi hiyo kuwapongeza mastaa wake ambao wamepambana hadi kufikia hatua hiyo ambayo haikutarajiwa na wengi huku akisisitiza safari moja huanzisha nyingine.

Alisema timu za Zanzibar msimu huu zilikuwa bora na zimeonyesha ushindani lakini wao ni bora zaidi na ndiyo maana wamefikia hatua hiyo ambayo wanaamini imeongeza morali kwa benchi la ufundi na wachezaji kuamini kila kitu kinawezekana.

“Wachezaji wangu wamekuwa wakihamasishana mazoezi wao ni bora hawatakiwi kumhofia mtu yeyote kwa sababu timu zote zinacheza na wachezaji 11 kama wao.”

Bares alisema baada ya kazi nzuri waliyoifanya mastaa wake amewapa mapumziko ya siku moja, kesho wataanza mazoezi ya kujiweka fiti tayari kwa mchezo wa fainali utakaochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Amaan.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live