Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlandege, Namungo ni bonge la mechi

Namungo Semi Znz Wachezaji wa Kikosi cha Namungo

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa soka visiwani hapa, leo wataendelea kupata burudani ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 wakati timu za Mlandege na Namungo zitakapopepetana kwenye bonge la mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo, huku makocha wa timu hizo wakitambiana mapema.

Pambano hilo limekuwa gumzo pengine kuliko nusu fainali ya kwanza iliyopigwa usiku wa jana kwa jinsi timu hizo zilizopenya hatua hiyo kimiujiza katika dakika za mwisho, Mlandege ikipenya kupitia Kundi C, ikiwa timu pekee ya Zanzibar kati ya sita zilizoshiriki michuano ya mwaka huu.

Namungo yenyewe ilifuzu kimiujiza mbele ya Aigle Noir iliyonyimwa penalti mbili za wazi ikiing'oa Chipukizi ya Pemba iliyokuwa ikiongoza kundi D na leo timu hizi zinakutana saa 2:15 usiku kuwania nafasi ya kwenda fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo tangu 2007.

Mlandege inayonolewa na Abdallah Mohammed 'Bares' mbali na kusaka nafasi ya kucheza fainali kwa mara ya kwanza katika misimu 17 ya michuano hiyo, lakini pia inataka kuzivua joho la unyonge timu za Zanzibar ikitaka kutinga fainali na hata kubeba taji kabisa.

Mara ya mwisho kwa timu ya Zanzibar kubeba ubingwa wa Mapinduzi ilikuwa 2009 wakati Miembeni ilipoinyoa Ocean View na mara ya mwisho kwa timu ya visiwani kutinga fainali ilikuwa 2012 kwa Jamhuri iliyocheza na Azam iliyobeba taji lake la kwanza kwa kuwapasua wenyeji kwa mabao 3-1.

Kocha Bares aliivusha Mlandege kwa kuifunga Simba ba 1-0 na kuitemesha taji, siku chache baada ya kutoka sare ya 1-1 na KVZ na kuongoza Kundi C, wakati Namungo ilianza na suluhu dhidi ya Chipukizi kisha kuifunga Aigle Noir iliyomaliza pungufu ya mchezaji mmoja kwa bao 1-0 na kuongoza Kundi D ikikusanya pointi nne ikifuatiwa na Chipukizi iliyokuwa na mbili na Warundi kukaa mkiani na pointi moja iliyotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Chipukizi.

Kocha huyo alisema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo licha ya kutambua ugumu atakaokutana nao uwanjani dhidi ya wapinzani wao wanaocheza nusu fainali yao ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kutolewa na Simba iliyoenda kubeba taji kwa kuichapa Azam bao 1-0.

“Nina watu wengi nyuma yangu ambao wananiangalia ni kwa namna gani nitaipambania Zanzibar kupeleka timu fainali. Wachezaji wangu wapo fiti na wana morali ya kuhakikisha wanafanya vizuri na hatimaye kutinga hatua hiyo,” alisema Bares na kuongeza;

“Naiheshimu Namungo, najua ni timu nzuri na yenye ushindani, ila nimejiandaa vizuri kuhakikisha timu yangu inapata matokeo chanya ndani ya dakika 90.”

Kocha wa Namungo, Denis Kitambi alisema kikosi chake kiko fiti na kina morali mzuri kuelekea mchezo huo wakitarajia ushindani ila ukweli wamejiandaa mapema kupigania nafasi yao ya kuandika rekodi ya kucheza fainali kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo ishiriki michuano hiyo.

Nyota wa kikosi cha Namungo, Shiza Kichuya alisema msimu huu nao wanautaka ubingwa kutokana na matokeo waliyoanza nayo, pia kwa ubora na uwezo wa wachezaji wote kwa jumla.

“Hata sisi Namungo malengo yetu ni ubingwa msimu huu, ndio maana tunapambana kila mechi kupata pointi, tumejipanga na tumeazimia kufikia ndoto, tunachoomba ni sapoti kwa mashabiki,” alisema Kichuya.

Winga huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Simba, aliongeza wanatarajia ushindani mkubwa lakini wamejiandaa kwa lengo la kupata matokeo mazuri na kutinga hatua ya fainali.

Chanzo: Mwanaspoti