Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwasa na sakata la kuitwa mwizi Simba

Boni Mkwasa Mkwasa na sakata la kuitwa mwizi Simba

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

"Kila nilipogusa mpira uwanjani walinizomea, wengine wakienda mbali zaidi wakiniita mwizii... mwiziiii, hali ile ilinivuruga, kuna muda hata kwenye kiwango changu iliniathiri," ndivyo anavyoanza kusimulia Charles Boniface Mkwasa katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake, Tegeta, Dar es Salaam.

Anasema ilikuwa ni kipindi cha mapito kwake, akikabiliana na mashabiki wa Simba, ambao kwa wakati ule waliamini Mkwasa amewaibia.

"Ilinivuruga, lakini nikajisemea moyoni, mimi sikuwaibia, pesa walinipa wenyewe, na pesa huwa haikataliwi, nakumbuka ilikuwa ni nyingi kwa wakati ule na kuna rafiki yangu mmoja tukiwa kambi ya Taifa Stars aliniambia, Boniface acha ujinga, chukua pesa hiyo.

"Nilipowafunga mara mbili wakaacha kunizomea ikawa nafuu kwangu," anasimulia Mkwasa akieleza mkasa wa usajili wake kwenye klabu ya Simba.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, katibu mkuu na kocha wa timu hiyo, anasema ilikuwa ni miaka ya 1980, Simba ilipomshawishi na kumsajili wakati huo akiwa Yanga.

"Walinifuata kambi ya timu ya Taifa, wakanirubuni kwa pesa, ilikuwa Sh45,000, wakati huo ni fedha nyingi sana, maana usajili wa wachezaji wa wakati huo ilikuwa ni Sh7000 au 8000, mimi nikamshirikisha rafiki yangu mmoja akasema hiyo pesa usiiache.

"Tulikubaliana wanipe pia nyumba ya kuishi, wakakubali, walinipa hundi ya Sh20,000 na fedha taslimu Sh25,000, nilijua ni siri kwa wakati huo, lakini haikuchukua muda ikavuja kuwa nimesaini Simba.

Anasema wakati sekeseke hilo likiendelea, walikwenda Kisumu kwenye mashindano, ambayo timu yao iliingia fainali, Mkwasa akiwa ndiye amesababisha mabao yote.

"El-Maamry (Said alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania, FAT, ambayo sasa ni TFF) alifurahi mno, akaja kunipongeza, palepale nikamwambi kiongozi nashukuru kwa pongezi, lakini mimi nikirudi nyumbani sichezi tena, haya ndiyo mashindano yangu ya mwisho.

"Akaniuliza kwanini? Nikamwambia nimesajili mara mbili, Simba na Yanga, hivyo nikirudi nafungiwa, wakati ule El Maamry alikuwa ni Simba damu, akaniuliza kwani wewe unataka kucheza timu gani? Nikamwambia kwa kuwa Yanga nimeizoea, bora nibaki Yanga.

"Akaniambia basi tukirudi Tanzania utacheza Yanga, hakuna wa kukufungia, sikuamini kwani alifanya uamuzi peke yake, hakukuwa na kikao wala nini," anasema Mkwasa.

CHIMBUKO LA JINA LA MKWASA

Anasema wakati huo alifahamika kama Charles Boniface, timu iliporejea nchini anasema Simba ilikuwa haijatimiza makubaliano ya kumpa nyumba kama walivyokubaliana.

"Tulikubalia wanipangie nyumba kubwa, wao wakanipeleka kwenye banda la uani, nilikuta tayari wamenihamisha nikamwambia mtu aliyekuwa nyumbani arudishe vitu kwenye nyumba tuliyokuwa tukiishi awali Kariakoo, akafanya hivyo.

"Waliponifuata nikawakana, nikawambia mimi siitwi Charles Boniface, mimi naitwa Charles Boniface Mkwasa, hela ya usajili hawakunipa mimi, nikakomaa kabisa mimi majina yangu ni haya matatu pale ndipo jina la Mkwasa lilipoanzia," ansema.

Alisimamia msimamo wake, Simba wakaizuia ile cheki ya Sh20,000 na akasalia na zile 25,000 ambazo hata hivyo baadaye aliwaambia kuwa angezirudisha.

"Anasema alitumia mbinu hiyo baada ya sakata la Yusuf Ismail, ambaye baadaye aliongeza jina la Bana, na yeye baada ya kuingia kwenye sekeseke na Simba akalikana la Charles Boniface na kudai yeye ni Charles Boniface Mkwasa huyo ambaye Simba ilimpa pesa hamfahamu.

"El Maamry alinisaidia sana, sikufungiwa na pesa sikurudisha, ingawa baadae niliwambia nitarudisha pesa, viongozi wakasema wao hawataki hela wanataka watu," anasema.

ALELEWA YANGA

Mkwasa aliiingia Yanga wakati klabu hiyo imefukuza nyota wengi kwenye mgogoro wa 1977, mwaka mmoja baadaye yeye na wachezaji wengine wakasajiliwa kwenye timu hiyo.

"Tulikuwa wadogo wadogo, nakumbuka tuliingia na kina Omary Hussein, marehemu Mkambi (Juma), Kinye (Hamis) na wengine tukaanza kutengeza timu, miaka minne baadaye timu yetu iliimarika tukamfunga Simba mfululizo," anasema Mkwasa, ambaye kabla ya kutua Yanga alicheza Tumbaku, Mseto na Reli za Morogoro.

Nyota huyo aliyewahi kuwa nahodha wa Taifa Stars kuanzia 1981-1985, alistaafu soka 1988, kisha Yanga ikampeleka kusomea ukocha nchini Brazil 1989.

"Walinichangia ada nikaenda kusoma, kabla ya kustaafu kucheza nilikuwa pia ni mhasibu wa Shirika la Ndege Tanzania kwa miaka 12, nilipokwenda Brazil nikarudi nikaona nijikite zaidi kwenye ukocha, nikaacha kazi Air Tanzania kutokana na maslahi, lakini pia nilizinguana na bosi wangu mmoja mwenye asili ya India, nikaacha kazi na kujikita kwenye ukocha," anasema.

ALIVYOFANYA KAZI NA MANJI

Mbali na Mkwasa kufundisha timu mbalimbali ikiwamo timu yake ya Yanga, aliwahi kuajiriwa kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, wakati wa uongozi wa Yusuf Manji.

"Manji aliniomba, aliona nimecheza, nimekulia Yanga, naifahamu, hivyo aliamini mimi ni mtu sahihi ninayeweza kumsaidia, aliponiambia sikusita, japo ilikuwa ni nafasi ngumu kuliko hata kuwa kocha," anasema.

Anasema ukiwa katibu unakuwa muwajibikaji, yeye alipoingia Yanga alikuta sakata la walioachishwa kazi bila kufuata utaratibu.

"Ilinibidi niende kama mshitakiwa mahakamani, ingawa kwa mujibu wa katiba baraza la wadhamini ndiyo lilipaswa kuwa mshitakiwa wa kwanza, lakini wakati huo huwezi kumpeleka mzee Katundu, nikalazimika kwenda mimi.

"Ni kazi yenye mambo mengi, mfano kutafua pesa ya kuendesha timu, nilipoingia pale hatukuwa na mdhamini, alikuwa ni Manji mwenyewe, nimekaa muda mfupi mwenyekiti akapata matatizo.

"Niliweka jitihada kubwa, kulikuwa na mgogoro wa Yanga na Azam na kuna pesa Yanga walizikataa, pia mgogoro wa kibiashara wa Manji na Azam, timu ikawa inapitia kipindi kigumu, nikapata wazo la kuishawishi Azam tuyamalize, niliongea na mwenyekiti, hakuwepo ofisini lakini akasema endelea tu.

"Baadaye tuliwapata SportPesa, mimi ndiyo nilisaini mkataba nao wa kwanza, ingawa kabla tulipitia kipindi kigumu baada ya Manji kupata matatizo.

"Watu wanakumbuka tulitembeza bakuli sana, nikapata wazo la kujaza kifusi hadi nikapewa jina la katibu wa kifusi, lengo lilikuwa kupunguza gharama za kulipa uwanja wa mazoezi, turudi Kaunda, tulipata michango kwenye makundi ya Yanga, kila kundi tuliomba litupe Sh200,000 yalikuwa yapo kama 100 hivi na zaidi.

"Azam pia tulirudisha uhusiano, wakatupa hela, ingawa ilikatwa kama Sh200 milioni na viongozi wetu wa mpira kwamba ni gharama za mechi ya Yanga na TP Mazembe, ambayo tulichezesha bila viingilio (hiyo mechi Manji alitangaza kiingilio ni bure kwenye Uwanja wa Taifa, sasa Mkapa).

"Kuna wakati hata mishahara tulikuwa tunapitisha muda, wiki mbili au zaidi, kama katibu nalazimika kuwambia wachezaji hali halisi, niilichofanya nakwenda Azam nawaomba mkopo, tunapewa pesa yetu ikitoka wanatukata mambo yanakwenda, wakati mwingine tunachangisha kwa wafanyabiashara wapenzi wa Yanga," anasema.

Anasema kila kilichokuwa kinafanyika, alikuwa akimshirikisha Mwenyekiti wa klabu (Manji) kila alipoata nafasi ya kuonana naye kipindi hicho akiwa kwenye matatizo.

Anasema licha ya changamoto ambazo Manji alipitia, lakini aliibeba klabu hiyo wakati wa uongozi wake na hadi anaondoka Yanga, pesa aliyoikopesha klabu hakuwa amelipwa.

"Alitoa pesa nyingi na hazikurudi hadi anaondoka Yanga, nikiwa katibu mkuu niliitwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kutoa maelezo ya namna klabu inavyoongozwa na Manji.

"Kuna habari zilipelekwa kwamba mwenyekiti anauza jezi hivyo anapata pesa nyingi kuliko anazotoa kwenye klabu, nikawambia hauzi jezi na hata klabu ikitaka pesa unaandikwa muhtasari wa kuomba pesa," anasema Mkwasa.

MIPANGO YA KUSTAAFU SOKA

Mkwasa ambaye baada ya kuondoka Yanga aliendelea na taaluma yake ya ukocha kwenye timu kadhaa ikiwamo ya Ruvu Shoorting, ambayo ameachana nayo miezi kadhaa iliyopita na kuamua kupumzika anasema hana muda mrefu wa kuwa kwenye mpira.

Anasema kufundisha klabu ni rahisi kuliko timu ya Taifa, kwani klabu ina mipango na mikakati yake, japo pia kuna changamoto kwa kocha aliyewahi kuwa mchezaji.

Anasema kwenye timu ya Taifa kuna changamoto hasa kwenye uwiano wa wachezaji, ukiita wengi kutoka Yanga au Simba, upande mmoja utaona kama si timu yao.

UNAHODHA WA SAMATTA

Mkwasa ndiye kocha aliyemteua Mbwana Samatta kuwa nahodha wa timu ya Taifa, jambo ambalo liliibua minong'ono ingawa mwenyewe anasema alifanya kwa sababu maalumu.

"Nakumbuka nilifanya hivyo tukiwa Zanzibar, sikufanya bila kumshirikisha Cannavaro (Nadir Haroub aliyekuwa nahodha wakati huo), nilimshirikisha ingawa baadaye alinikana akasema hajaambiwa na mimi kupata changamoto kubwa na watu wakihoji kwanini nimefanya hivyo.

"Ingawa nilifanya vile kwa makusudi, niliona Samatta ndiye nembo yetu kwenye soka na lazima tumpe majukumu na heshima yake, nashukuru mtazamo wangu ukawa ni huo hadi leo bado ni nahodha," anasema.

Anasema tatizo la Tanzania, kila shabiki wa mpira ni kocha mzuri, kiongozi, mwamuzi na mchezaji mzuri, hivyo watu wanataka ukipanga timu, upange wanayoitaka wao sio kwa uwezo na profesheno yako kocha.

MTAZAMO WAKE

Mkwasa anasema soka nchini linapanda kwa ngazi ya klabu na si kwenye timu ya Taifa, ambako matokeo si mazuri kutokana na wazawa kutopata uzoefu.

Chanzo: Mwanaspoti