Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwasa ataja sababu ya kusepa Ruvu Shooting

Mkwasa.png Mkwasa ataja sababu ya kusepa Ruvu Shooting

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa, ametangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo ambayo imecheza mechi 10 mfululizo bila kupata ushindi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkwasa alisema ameamua kukaa kando baada ya kuona falsafa anazozitoa kwenye kikosi chake hazieleweki vema na wachezaji, hivyo kuifanya timu hiyo isifanye vizuri.

Mkwasa ameamua kubwaga manyanga siku mbili tu baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, Jumamosi, akiwa ameiongoza timu hiyo mechi zote za mzunguko wa kwanza, ikishinda  tatu, sare mbili na kupoteza michezo 10.

"Tumejitahidi kufundisha, nimejitahidi kuweka falsafa, lakini kila tukiingia kuna makosa yanafanywa tunafungwa, labda falsafa zangu hazieleweki vema, kwa hiyo nimeamua kukaa pembeni ili atafutwe mtu ambaye anaweza kuendelea nayo. Maana kushindana ni kwamba ushinde na wewe ushindwe, lakini kushindwa kila mechi ni tatizo," alisema Mkwasa.

Mara ya mwisho Ruvu Shooting kushinda ilikuwa Septemba 29, mwaka huu ilipoichapa Coastal Union mabao 2-1, lakini baada ya hapo imecheza mechi 10 mfululizo bila kupata ushindi, ikifungwa nane na sare mbili.

Baada ya kupata ushindi dhidi ya Coastal, ilichapwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, ikatoka suluhu dhidi ya KMC, ikapokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Kagera Sugar na ikafungwa kwa idadi hiyo hiyo ya mabao dhidi ya Gaita Gold.

Kama vile haitoshi ikaruhusu kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Baada ya sare hiyo, Ruvu Shooting ikapokea vipigo vingine vinne mfululizo na kumfanya Mkwasa aamue kujiweka kando, ambavyo ni dhidi ya Azam ilifungwa bao 1-0, ikararuriwa mabao 4-0 dhidi ya Simba, bao 1-0 dhidi ya Singida Big Stars, kabla ya Jumamosi kupoteza tena 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji.

Timu hiyo ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 11 na tayari imemaliza mechi zake15  za mzunguko wa kwanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live