Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwasa ainyooshea kidole safu ya ushambuliaji Ruvu Shooting

Mkwasa.png Mkwasa ainyooshea kidole safu ya ushambuliaji Ruvu Shooting

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amewatupia lawama washambuliaji wake kwa kukosa umakini katika kutumia nafasi za kufunga mabao walizozipata dhidi ya Kagera Sugar huku nyota hao wakifanya makosa ambayo yaliwanufaisha wapinzani wao.

Ruvu Shooting ilikubali kichapo cha mabao 2-1 ugenini Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa huku mabao ya wenyeji yakifungwa na Hamis Kiiza dakika ya tisa na Anuary Jabir dakika ya 69 wakati bao la kufutia machozi la Ruvu likipachikwa na Rashid Juma.

Baada ya kichapo hicho Ruvu Shooting inakamata nafasi ya sita ikiwa na pointi 10 huku Kagera Sugar ikisogea hadi nafasi ya 12 ikifikisha pointi nane baada ya kushinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Polisi Tanzania na Ruvu Shooting.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkwasa alisema wachezaji wake walitengeneza nafasi nyingi za mabao lakini walikosa umakini katika kuzitumia huku wakishindwa kufanya maamuzi ya haraka wanapolifikia lango la mpinzani na kujikuta wamepokonywa mipira.

“Wenzetu wamekuja na nguvu na kujiamini, wametumia nguvu yao na nafasi ya mapema waliyoipata, lakini tulijitahidi kutumia nafasi japo tulifanikiwa lakini baadaye tukapoteza mwelekeo wakapata bao la pili kwahiyo niwapongeze wameshinda lakini na sisi tulipata nafasi kadhaa ambazo hatukuzitumia.

“Kikubwa kilichotuangusha ni matukio ya kufikiri kwa haraka kwa sababu tulipata nafasi nyingi za kufunga tuka-delay wakatupokonya mipira kwahiyo ni makosa ya kibinadamu na kiutawala kwa mchezaji,”

“Sasa tutarudi kufanyia kazi pale tulipoteleza na kuhakikisha tunafuta makosa na kurudi tukiwa bora zaidi kwenye mchezo ujao,” alisema Mkwasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live