Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwasa, Pawasa, Mwaisabula waishangaa Simba

Mkwasaa Ed Mkwasa, Pawasa, Mwaisabula waishangaa Simba

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: Dar24

Makocha wa soka nchini Boniface Mkwasa, Kenny Mwaisabula na Boniface Pawasa wameukosoa Uongozi wa Simba SC kwa kufanya maamuzi ya kumtimua Kocha Robertinho.

Uongozi wa Simba SC ulifikia maamuzi hayo jana Jumanne (Novemba 07), baada kikosi chao kikubali kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Young Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pia, taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Imani Kajula, ilieleza kocha wa viungo Corneille Hategekimana raia wa Burundi, naye amefutwa kazi, huku ikielezwa katika kipindi cha mpito kocha mkuu atakuwa Daniel Cardena akisaidiwa na Selemani Matola.

Robertinho amepoteza mechi moja kati ya saba za Ligi Kuu Tanzania Bara na kuipeleka Simba SC katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, aliyekuwa kocha wa Young Africans, Ruvu Shooting na timu ya taifa Taifa Stars, Charles Mkwasa, amesema klabu hiyo imechukua uamuzi wa haraka kumtimua kwa kuwa kocha huyo amekuwa na matokeo mazuri msimu huu.

“Kocha kapoteza mchezo mmoja tu, haikuwa sawa kuachana naye mapema hivi, lakini inawezekana mkataba wake ulikuwa unasema hivyo,” amesema Mkwasa.

Kwa upande wa Kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni na beki wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars, Boniface Pawasa, amesema uongozi wa klabu hiyo haujachukua uamuzi sahihi kumuondoa Robertinho, isipokuwa alidai aliyepaswa kung’olewa ni kocha wa viungo.

“Kwa upande wangu sijaona kama ni sahihi kuachana na kocha mkuu. Kocha wa viungo ndiye alistahili kuondoka kwa sababu wachezaji wa Simba SC hawana pumzi ya kutosha,” amesema.

Naye, Kennedy Mwaisabula ambaye aliwahi kuwa kocha wa Young Africans, amesema haukuwa wakati sahihi kwa klabu ya Simba kumtema Robertinho kwa sababu matokeo aliyopata dhidi ya watani wao wa jadi ni ya kawaida katika soka.

“Inawezekana ni makubaliano yao ambayo walikubaliana, lakini kwa upande wangu haukuwa uamuzi sahihi, (Simba) walitakiwa kukaa naye na kuzungumza kwa kuwa ni mechi yake ya kwanza kupoteza (msimu huu),” amesema.

Robertinho alitua Simba SC Januari 2023, akitokea Vipers ya Uganda. Katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita 2022/23, Mbrazili huyo aliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili na kuishia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Dar24