Umeona msimamo wa Ligi Kuu England ulivyo. Arsenal ipo kileleni na pointi 69. Baada ya hapo unashuka nafasi ya pili, tatu, nne, tano, sita, saba, nane, tisa bado hautawaona Chelsea. Utashuka hadi nafasi ya 10 huko, ndiyo utawaona wakali hao wa Stamford Bridge.
Ndiyo namba 10. Pointi 31 nyuma ya kuwafikia Arsenal. Pointi 11 nyuma ya kuifikia Tottenham Hotspur waliopo kwenye Top Four.
Lakini, unaambiwa hivi, kocha wa Chelsea, Graham Potter anashika namba nne kwa kulipwa pesa nyingi duniani, akiwazidi makocha wengi akiwamo Carlo Ancelotti wa Real Madrid. Ndiyo hivyo, usishangae, kocha huyo wa zamani wa Brighton, analipwa pesa nyingi kuliko hata The Special One, Jose Mourinho.
Potter, ambaye amekuwa kwenye wasiwasi mkubwa wa kibarua chake huko Stamford Bridge kutokana na Chelsea kufanya hovyo, yeye analipwa pesa nyingi kuliko hata mtangulizi wake, Thomas Tuchel kwa kiwango anacholipwa huko kwenye ajira yake mpya Bayern Munich.
Kwa mujibu wa takwimu za gazeti la Ufaransa la L’Equipe, makocha watatu kati ya wanne wanaoongoza kwa kulipwa mkwanja mrefu, wanafanya kazi kwenye Ligi Kuu England.
Potter anaripotiwa kuweka mfukoni Pauni 11,917,404 kwa mwaka.
Kwa kugawa pesa hiyo, ina maana Potter anakwenda nyumbani na Pauni 993,117 kila mwezi, sawa na Pauni 229,180 kila wiki.
Wakati mfukoni akiwa vizuri, Potter ameanza maisha yake huko Chelsea kwa ugumu kutokana na timu hiyo kushindwa kupiga hatua yoyote kwenye ligi tangu alipoondoka Tuchel, kutokana na timu kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.
Katika mechi zake 30 alizoiongoza timu hiyo, ameshinda 12 tu, sare nane na vichapo 10.
Ni makocha wa Diego Simeone wa Atletico Madrid, Pep Guardiola wa Manchester City na Jurgen Klopp wa Liverpool ndio wanaolipwa pesa nyingi kumzidi Potter.
Simeone ndiye anashika namba moja akiweka kibindoni Pauni 29.8 milioni kwa mwaka.
Guardiola yupo kwenye nafasi ya pili, akilipwa Pauni 19.7 milioni kwa mwaka na Klopp anakamilisha tatu bora, akivuna Pauni 15.7 milioni kwa miezi 12.
Baada ya Potter kwenye nafasi ya nne, anayefuata ni kocha wa Juventus, Max Allegri, anayelipwa Pauni 11.3 milioni kwa mwaka, huku Tuchel akiibukia kwenye nafasi ya sita kutokana na Bayern Munich kumlipa Pauni 10.5 milioni katika kila baada ya miezi 12.
Kitu cha kushangaza, mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Carlo Ancelotti anashika namba saba akiwa analipwa Pauni 9.6 milioni, huku kwenye namba nane na tisa wapo Simone Inzaghi wa Inter Milan na Jose Mourinho wa AS Roma mtawalia. Inzaghi analipwa Pauni 8.8 milioni kwa mwaka, wakati Mourinho anapokea Pauni 8.1 milioni kwa miezi 12.
Anayekamilisha orodha ya makocha 10 wanaolipwa pesa ndefu duniani ni jina linaloshangaza, Xabi Alonso - ambaye kwa kazi yake anayofanya huko Bayer Leverkusen, inamlipa Pani 4.4 milioni kwa mwaka.
Orodha ya gazeti hilo la Ufaransa inafichua kwamba kocha wa Wolfsburg, Niko Kovac yupo kwenye nafasi ya 11, akilipwa Pauni 3.5 milioni kwa mwaka, akimzidi kidogo sana Xavi wa Barcelona, anayelipwa Pauni 3.4 milioni kwa mwaka.