Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkufunzi wa waamuzi ashangaa bao la Simba

94669 Simba+pic Mkufunzi wa waamuzi ashangaa bao la Simba

Thu, 6 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bao la nahodha wa Simba John Bocco alilofunga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania, limeibua mjadala.

Bocco alifunga bao linalodaiwa la utata katika mchezo ambao Simba ilishinda mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi.

Bao la mshambuliaji huyo limeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na vijiwe mbalimbali vya mashabiki wa soka wakidai Bocco alikuwa ameotea kabla ya kufunga.

Pia wadau wa michezo walitoa maoni kuhusu uhalali wa bao hilo akiwemo mkufunzi wa waamuzi nchini, Omari Abdulkadir ambaye alisema halikuwa halali.

Abdulkadir ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), alisema Bocco alikuwa katika eneo la kuotea kabla ya kufunga dakika ya 57.

Alisema mwamuzi Hans Mabena wa Tanga alishindwa kutafsiri vyema sheria za soka kwa kukubali bao hilo ambalo lilikuwa la kusawazisha kwa Simba.

Pia Soma

Advertisement
Nguli huyo alisema kiwango cha soka kinadumazwa na baadhi ya waamuzi ambao kwa kujua au kutokujua wanashindwa kutafsiri vyema sheria za soka hatua aliyosema ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya soka nchini.

“Ile ilikuwa ni offside ya wazi sijui kwanini waamuzi wa aina hiyo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) inawafumbia macho,” alisema Abdulkadir alipozungumza na gazeti hili jana.

Alisema kuna tatizo katika mfumo wa soka la Tanzania ambao unachangiwa na baadhi ya watu wakishirikiana na waamuzi kwa lengo la kuvuruga mpira kwa maslahi yao binafsi.

“Kuna mambo ya kushangaza katika mpira, hivi sasa baadhi ya waamuzi wanatoa uamuzi wa kushangaza kwa nini hawafungiwi kabisa,” alisema Abdulkadir.

Mwamuzi mstaafu na mkufunzi wa waamuzi Leslie Liunda alisema kuna tatizo katika eneo la uamuzi ambalo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.

“Tunapaswa kujua tatizo liko wapi, mahali gani tunakosea kwani haijawahi kutokea hivi, si vizuri kukurupuka kusema lakini ni lazima kutafuta chanzo na bahati nzuri ni kwamba hakuna tatizo ambalo halitatuliki pale utakapobaini,” alisema Liunda.

Wakati Abdulkadir na Liunda wakitoa maoni hayo, Mwenyekiti wa FRAT, Joseph Mapunda aligoma kuzungumzia suala hilo akidai maadili ya Fifa, CAF na TFF hayaruhusu kwa kuwa jukumu hilo lipo kwa kamati ya waamuzi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Salum Chama alisema leo Alhamisi watatoa tamko baada ya kikao cha ndani kujadili ripoti ya mchezo huo.

“Kesho (leo) tuna kikao nitazungumzia bao la Simba la jana (juzi),” alisema Chama kwa kifupi.

Mbali na mechi ya Simba, mechi nyingine tano ambazo ziliibua mjadala kutokana na uamuzi wenye utata ni ile baina ya Azam dhidi ya Mtibwa iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Azam ikisawazisha dakika ya 90.

Yanga na Coastal Union iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0, Simba na Mwadui Simba ikishinda mabao 2-1. Pia Simba na Namungo iliyomalizika kwa Simba kushinda mabao 3-2.

Chanzo: mwananchi.co.tz