Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkude, kila enzi zina mwisho wake

Jonasmkude20 Mkude, kila enzi zina mwisho wake

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni ngumu sana kufikiri. Ni ngumu pia kuamini. Baada ya miaka 13 ndoa ya Jonas Mkude na Simba imevunjika. Ni huzuni sana.

Siku zote watu hufahamu mwanzo wao lakini mwisho huwa mgumu sana. Ni Kama alivyoimba mwanamuziki nguli, Celine Dion. “It is sad to say goodbye”. Ni kweli. Ni ngumu sana kusema kwaheri.

Ni ngumu kwa Simba. Ni ngumu kwa Mkude. Ila ukweli ni kwamba kila zama huisha. Kila Falme hupita. Kila nyakati hubadilika.

Pengine watu wengi hawakuwaza kama ingekuwa sasa kwamba Simba ingeachana na Mkude. Ila wamefanya maamuzi magumu. Wameamua kuanza upya. Si jambo jepesi hata kidogo. Naamini iliwachukua muda sana viongozi wa Simba kufanya maamuzi haya.

Mkude alikuwa kipenzi cha Wanasimba. Hawakujali kama anacheza ama la. Waliimba na kusifu jina lake kila siku. Walimpenda sana. Unatokaje hadharani na kuwaambia kuwa anaondoka klabuni hapo? Ni ngumu.

Baada ya Ulimboka Mwakingwe kudumu Simba kwa miaka tisa, ni Mkude pekee ameweza kuvunja rekodi hiyo. Ulimboka alikuwa fundi haswa. Pamoja na utukutu wake aliweza kukaa Msimbazi pale kwa miaka hiyo tisa.

Si jambo jepesi hata kidogo. Simba wamepita mafundi wengi sana. Tangu enzi za kina Zamoyoni Mogella, Malota Soma, Steven Mapunda na wengineo. Hakuna aliyeweza kudumu Simba kwa muda mrefu kama Mkude.

Pale Yanga ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliweza kudumu kwa muda mrefu zaidi. Alicheza pale kwa miaka 11. Akashinda mataji kadhaa. Akaacha alama zake pale.

Cannavaro aliweza kufanya hivyo kutokana na nidhamu yake. Aliweza kutunza kipaji chake. Alijituma katika kila mechi. Yanga ilimtegemea. Taifa Stars ilimtegemea. Ila ilifika wakati Cannavaro akaona imetosha. Akaamua kutundika daluga pale Yanga. Alikubali kuwa zama zake zimekwisha.

Haikuwa kazi nyepesi kwa Mkude kudumu miaka hiyo 13 pale Simba. Walikiona kipaji chake akiwa kijana mdogo tu. Wakati anapewa nafasi kikosi cha wakubwa mwaka 2011 hawakuwa na hisia kama hizi. Hawakujua kama angedumu kiasi hicho.

Bahati mbaya kwa Mkude katika miaka yake mingi pale Simba alikumbwa na skendo. Kuna watu walipenda zaidi kuzungumza mabaya yake kuliko mazuri. Wanachoshindwa kusema ni kwamba Mkude pamoja na shida zake alijua kulinda kipaji chake.

Umewahi kujiuliza kwanini hao wachezaji wengine waliokuwa na nidhamu. Waliokuwa na vipaji vikubwa kuliko Mkude. Kwanini hawakudumu Simba kwa muda mrefu kama yeye? Hili hawasemi.

Mkude pamoja na yote alikuwa bora uwanjani. Angewakera nje, lakini ndani ya Uwanja angekupa kitu bora. Ndio sababu kwa miaka nenda rudi kuna timu zilitamani kumsajili lakini alichagua kubaki Simba.

Ila ndio hivyo. Nyakati huisha. Hata mafundi wa mpira pia huachwa zama zao zikiisha. Sio kwamba Simba hawampendi Mkude, ila ni zama tu zimepita.

Ndio sababu Ronaldinho Gaucho aliondoka pale Barcelona baada ya zama zake kuisha. Nani aliwaza kama Xavi Hernandez na Andres Iniesta wangeondoka Barcelona? Hakuna. Wengi walidhani kama wangemalizia soka lao pale. Ila waliondoka. Ilikuwa mwisho wa enzi.

Iniesta alikesha kwa machozi ndani ya Camp Nou katika siku yake ya mwisho. Haikuwa rahisi kwake kuamini Kama anaondoka. Hakukuwa na namna. Zama zake ziliisha.

Ni kama ilivyokuwa kwa Lionel Messi ndani ya Barcelona. Ilifika wakati ndoa yao ikashindwa kuendelea. Alimwaga machozi mbele ya wanahabari. Ila aliondoka. Ni ngumu sana. Nadhani wakati huu Mkude anaondoka ni vyema tukasifu enzi zake pale Simba.

Baada ya yeye kupandishwa timu ya wakubwa, walikuja vijana wengi wenye vipaji vikubwa. Kina Ramadhan Singano, Said Ndemla, Ibrahim Ajib, William Lucian, Khatib Juma, Ibrahim Isihaka na wengine kibao. Wote waliondoka ila Mkude alibaki.

Wamepita makocha zaidi ya 10 katika enzi zake pale Simba na wote walimtumia. Si jambo jepesi kumshawishi kila kocha. Ila Mkude aliweza. Anastahili pongezi kubwa sana.

Nasikia Yanga wanamtaka. Si kitu cha kushangaza. Wapo wachezaji wakubwa walimalizana na timu zao kisha wakaenda timu nyingine kubwa. Messi alikwenda PSG. Edibily Lunyamila alikwenda Simba. Mifano ni mingi sana. Ni kama Sure Boy alivyoondoka Azam FC baada ya miaka 12 akaenda Yanga na bado anakiwasha. Ndio mpira wa miguu ulivyo.

Kitu kizuri ni kama kweli Simba itamuaga kwenye Tamasha la Simba Day baada ya mabosi wa klabu hiyo kuamua kuvaa mabomu kutokana na mashambulizi ya wadau wa soka waliowasakama kwa kumpa 'Thank You' kihuni!

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: