Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkude anavyojiheshimisha Simba, Yanga

Mkude Simba Ss Kiungo wa Yanga Jonas Mkude

Mon, 22 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo wa Yanga, Jonas Mkude 'Nungunungu' amejiwekea rekodi ya kipekee baada ya kucheza 'Dabi ya Kariakoo' akiwa na timu zote mbili bila ya kupoteza.

Mkude aliyejiunga na Yanga msimu huu baada ya kuachana na Simba aliyoichezea kwa misimu 12, ameweka rekodi ambapo katika michezo sita iliyopita ya Ligi Kuu Bara aliyohusika kwenye timu hizo zote kubwa hakuna aliyopoteza zaidi ya ushindi au sare.

Katika michezo hiyo sita, minne aliichezea Simba na kati yake alishinda mmoja huku mingine mitatu iliyobaki ikiisha kwa sare.

Dabi za sare zilikuwa za 0-0, Desemba 11, 2021, 0-0, Aprili 30, 2022 na 1-1, Oktoba 23, 2022 ambapo zote alianza katika kikosi cha kwanza wakati mechi ya ushindi ilikuwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga iliyopigwa Aprili 16, mwaka jana aliyoanzia benchini.

Katika michezo hiyo yote akiwa na Simba, Mkude alifundishwa na makocha watatu tofauti akianza na Mhispania, Pablo Franco aliyeongoza dabi mbili, akafuata Juma Mgunda huku wa mwisho kwake akiwa ni Mbrazili, Robertinho Oliveira 'Robertinho'.

Akiwa na Yanga amehusika katika dabi zote mbili ambapo timu hiyo imeshinda zote ikianza na ushindi wa mabao 5-1, Novemba 5, mwaka jana alipoingia katika dakika ya 88 akichukua nafasi ya Mudathir Yahya na ile ya 2-1, iliyopigwa wikiendi iliyopita ya Aprili 20, mwaka huu.

Pia ameingia katika rekodi akiwa ni mchezaji ambaye timu zote alizocheza zilishinda mabao matano kwenye mechi ya dabi ya Kariakoo.

Mkude alianza kufanya hivyo akiwa na Simba walipoifunga Yanga mabao 5-0, Mei 6, 2012 kisha akafanya tena wakati akiwa na Yanga msimu huu walipoifunga Simba 5-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Novemba 5, mwaka jana.

Nyota huyo alikaririwa akieleza anajisikia furaha kuandika rekodi hiyo muhimu huku akijivunia kucheza michezo mingi ya dabi.

"Dabi ya Kariakoo iliyochezwa Aprili 20, mwaka huu ilikuwa ni ya 32 kwangu, hivyo ni kitu kikubwa ninachojivunia sana," alisema.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: