Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Yanga, George Mkuchika amesema kama timu hiyo isingenyimwa bao la nyota wa kikosi hicho, Stephane Aziz KI wakati wa mechi yao ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns wangefika mbali zaidi.
Mkuchika amezungumza hayo leo wakati wa Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo unaofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
"Lile bao lilinisikitisha sana na kama sio yale yaliyotokea basi naamini tungefika mbali zaidi ya robo fainali ila ipo siku tutaleta taji la Afrika hapa nchini," amesema.
Mkuchika aliongeza, Yanga itakuwa timu ya kwanza kuleta taji la Afrika na itakapofanya hivyo italipeleka moja kwa moja kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kama ishara ya kumshukuru katika mchango wake kwenye sekta ya michezo.
Bao hilo lilizaa utata mkubwa wakati Yanga ikicheza mechi ya mkondo wa pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns uliopigwa Aprili 5, mwaka huu jijini Pretoria baada ya miamba hiyo kutoka suluhu katika mechi zote mbili.
Kitendo cha mwamuzi wa mchezo huo, Beida Dahane kutoka Mauritania kukubaliana na ushauri wa waamuzi wa chumba cha VAR, uamuzi wake ulikosolewa na mashabiki wengi wakiona haukuwa sahihi.
Mtazamo wa Mkuchika katika bao la Aziz Ki, unafanana na wa Rais wa CAF, Patrice Motsepe, ambaye pia ni mmiliki wa klabu ya Mamelodi, kwamba Yanga ilinyimwa haki katika mechi ile iliyochezwa nchini Afrika Kusini.
Motsepe aliyetua hapa nchini hivi karibuni alinukuliwa akisema; "Ingawa Rais wa CAF hatakiwi kutoa maoni kuhusu uamuzi wa waamuzi, lakini kwangu binafsi nilivyorudia kuangalia lilikuwa ni bao halali lakini naheshimu sana taratibu zote za waamuzi na tuna jukumu la kutakiwa kulinda na kuheshimu uamuzi wa waamuzi na mechi kamishna wa michezo kwa afya ya soka letu."