Gwiji wa Simba na nyota wa kimataifa wa zamani wa Tanzania, Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ameshindwa kujizuia na kuweka bayana matamanio ya kutaka kurudi kwenye klabu hiyo aliyoichezea na kuifundisha kwa nyakati tofauti.
Kibadeni anayeshikilia rekodi ya kufunga hat trick katika mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga 1977, aliliambia Mwanaspoti kuwa anatamani kurudi, lakini safari hii akiwa tofauti.
“Kama uongozi utaridhia wanirudishe niwe meneja au hata mshauri tu wa ufundi, maana hizo ndizo nafasi zetu kwa sasa,” alisema Kibadeni katika mahojiano maalumu na gazeti hili.
Alisema anatamani kurudi kwenye klabu hiyo kwa kuwa inamhusu.
“Sio kunihusu tu, lakini inanihusu sana. Naumia nikiona vile inapata shida ya kiufundi wakati kuna mambo mengine sisi wachezaji wake wa zamani elimu ya kusaidia tunayo,” alisema Kibadeni aliyeichezea Simba miaka ya 1970 kabla ya kutimkia Majimaji 1978.
“Huwa naona kwa nini nisipate nafasi ya kusaidia. Napenda sana kurudi Simba, basi hata niwe mshauri wa kocha. Nipate tu fursa ya kuwa kwenye benchi la ufundi. Ili niwemo kwenye timu ikitokea limepungua jambo basi tunashauri. Klabu ikipokea ombi langu nitafurahi sababu naipenda Simba na ni klabu ambayo inanihusu tangu nikiwa kijana.”
Akizungumzia ndoto ya Kibadeni, nyota mwingine wa zamani wa Nyota Nyekundu na Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema mkongwe huyo anastahili.
“Sio kufaa tu anafaa sana, nchi nyingine huwa haziwaachi moja kwa moja wachezaji wake wa zamani na zinanufaika nao,” alisema.
Kwa Simba nahodha wa zamani wa timu hiyo, Suleiman Matola ni kocha msaidizi ambaye sasa ana kaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya Pablo Franco kutimuliwa.
“Ni vizuri klabu kama Simba kuwa na kocha Mzungu kwa kuwa Mzungu ni Mzungu tu, lakini inapokuwa kwenye benchi na mchezaji wa zamani wa timu aliyewahi kuitumikia kwa mafanikio ni jambo zuri sana. Wale ndio wanalifahamu soka la Afrika, hivyo wanakuwa wakisaidia kujenga timu,” alisema Bwalya.