Siku moja baada ya klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro kumtambulisha mshambuliaji Deo Kanda kuwa staa wao mpya, klabu ya Kitayosce ya Tabora imeibuka vikali ikidai Mkongomani huyo ni mchezaji wao halali.
Mapema Kitayosce ilimshusha Kanda nchini akitokea kwao DR Congo tayari kwa usajili wa kutua kwenye klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championiship.
Wakati Kanda akisubiriwa kuonekana Kitayosce, ghafla juzi alitambulishwa na Mtibwa Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Bara kuwa imemnasa winga huyo mkongwe wa zamani aliyewahi kuzitumikia TP Mazembe na Simba.
Mmiliki wa Kitayosce, Yusuf Kitumbo ameliambia Mwanaspoti kwamba wameshtushwa na hatua ya Mtibwa kumtambulisha Kanda hali ya kuwa wao ndio waliomleta nchini wakimfuata kwao jijini Lubumbashi nchini Congo akiwa kama mchezaji aliyeachana na soka.
“Sisi (Kitayosce) ndio tulimfauata Kanda kwao kijijini Lubumbashi akiwa anafanya shughuli nyingine sio za kimpira tukiamini kwa ukongwe wake ataweza kuja kutusaidia na tukakubaliana karibu kila kitu,” alisema Kitumbo.
“Baada ya mazungumzo akasaini mkataba wetu halali (Mwanaspoti imeona nakala yake) akachukua fedha zetu mbalimbali za ada ya usajili, alitaka aache fedha kwao tukampatia, tukamlipia ada ya vipimo vya uviko 19 na tiketi ya ndege mara ya kwanza akashindwa kusafiri tukalipia tena gharama za kuirudisha ile tiketi hakusafiri tena.
“Mara ya mwisho ndio akasafiri na kufika nchini lakini mpaka anafika hapa tayari alishatugharimu fedha nyingi akiwa tayari alishachukua sehemu ya fedha zake za usajili.”
Aidha, Kitumbo aliongeza baada ya kufika nchini Kanda ambaye aliwahi kucheza fainali za Kombe la Dunia za klabu akiwa na Mazembe aligoma kusafiri kuelekea Tabora kujiunga na timu akitaka mambo mawili yafanyike.
“Tulipomwambia aje Tabora akagoma akaanza shida sisi tulishtuka tukamuuliza nini tatizo akasema yeye sio mchezaji wa kucheza klabu ndogo na anataka kujiunga na DTB, tukamuuliza DTB na Kitayosce zina tofautiana nini?
“Bahati nzuri sisi Kitayosce tuna uhusiano mzuri na DTB, kiongozi wao alitupigia na akatueleza kuwa anataka kumchukua Kanda, tukamweleza kwa ushahidi kwamba huyu ni mchezaji wetu, lakini alipofika hapa ameanza kutusumbua,bahati nzuri DTB waliiona shida na wakasitisha mpango wao.
“Baada ya hapo akaja na masharti mengine kwamba kabla ya kwenda Tabora anataka amaliziwe fedha zake za usajili ambazo hazikuwa shida kwetu fedha zilizobaki ni kidogo lakini sharti la pili akataka tumlipe mishahara yake ya miezi sita kwa pamoja kabla ya kuanza kazi,tukaona hapa kuna shida.”
Mkurugenzi wa Utawala wa Mtibwa Sugar, Swabti Abubakar alisema wamenasa saini ya mchezaji huyo baada ya kufuata taratibu zote.