Kipa mpya wa Kagera Sugar, Mkongomani Alain Ngeleka amesema anahitaji muda zaidi kwenye kikosi hicho kutokana na ushindani uliopo mbele ya makipa wenzake Ramadhan Chalamanda na Said Kipao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngeleka alisema licha ya ubora alionao, lakini haitakuwa rahisi kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza hivyo ana kazi kubwa ya kufanya ili kulishawishi benchi la ufundi.
“Naamini katika kipindi hiki ambacho tunacheza michezo ya kirafiki ndicho ambacho natumia kwa ajili ya kuonyesha uwezo wangu,” alisema kipa huyo.
“Nawaheshimu wenzangu hivyo jukumu kwangu ni kupambana.”
Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi hicho, Mecky Maxime alisema ushindani unapokuwepo katika kila nafasi kikosini ni jambo nzuri kwani unaiweka timu kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri zaidi kuliko kumtegemea mtu mmoja.
“Kila mchezaji ana nafasi sawa na mwenzake ila kitakachowatofautisha ni kwa yule atakayejituma zaidi,” alisema Maxime.
Ngeleka amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na Kitayosce (Tabora United) wakati ikishiriki Championship kabla haijapanda Ligi Kuu Bara kufuatia kumsajili akitokea klabu ya Lumwana Radiant ya nchini Zambia.
Timu nyingine alizowahi kucheza ni Nkana na Buildcon zote za Zambia, Sanga Balende, Groupe Bazano na Tshinkunku za kwao DR Congo.
Kagera Sugar imecheza mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Mashujaa na Ihefu, na mchezo ujao wa michuano hiyo inatarajiwa kuikaribisha Geita Gold katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.