Mlinzi katika uwanja wa Lusail amefariki dunia baada ya kuanguka kutoka uwanja wa Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya ushindi wa Argentina wa robo fainali dhidi ya Uholanzi.
Mkenya John Njau Kibue awali alisemekana kuwa katika hali nzuri lakini mbaya - hata hivyo, alifariki baada ya siku tatu hospitalini.
Waandalizi wa Qatar wanasema "wanachunguza hali iliyopelekea kuanguka kama jambo la dharura".
Dadake mwenye umri wa miaka 24 aliiambia CNN kuwa hawajapewa maelezo.
"Tunataka haki. Tunataka kujua kilichosababisha kifo chake. Hawajawahi kututumia picha ya kuonyesha alikoanguka au kutupa taarifa nyingine," Ann Wanjiru alisema.
Familia ya Kibue iliiambia CNN kwamba alihamia Qatar mnamo Novemba kufanya kazi kwa kandarasi na kampuni ya usalama ya eneo hilo.
Kibue ni mfanyakazi wa pili mhamiaji aliyeripotiwa kufariki tangu kuanza kwa Kombe la Dunia tarehe 20 Novemba.
Raia wa Ufilipino alifariki dunia alipokuwa akifanya ukarabati katika eneo la mapumziko linalotumiwa kama kituo cha mazoezi cha timu ya Saudi Arabia, gazeti la The Athletic liliripoti.
Wakati kamati kuu ya mashindano hayo ikisisitiza kwamba kifo hicho kilitokea kwenye eneo lililo nje ya mamlaka yake, ilisema ilitoa "rambirambi za dhati" kwa familia ya Kibue, wafanyakazi wenzake na marafiki.
Ripoti ya gazeti la Guardian mwaka jana ilisema wafanyakazi wahamiaji 6,500 wamefariki dunia nchini Qatar tangu nchi hiyo ilipotunukiwa Kombe la Dunia mwaka 2010.
Hata hivyo hilo limekanushwa na mamlaka za Qatar, zinazosema kumekuwa na vifo vitatu kutokana na ujenzi vinavyohusiana moja kwa moja na kwenye mashindano hayo, na vifo vingine 37 visivyohusiana na kazi.