Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke asimulia dakika za mwisho za Gidabuday

Gidabuday Wife Mke asimulia dakika za mwisho za Gidabuday

Thu, 12 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

"Nilipigiwa simu na mtu ambaye aligoma kujitambulisha ni nani, na hadi leo sijamfahamu akaniambia mume wangu amegongwa na gari amefariki," anaanza kusimulia Eva Baltazar, mke wa katibu mkuu mstaafu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday.

Gidabuday alifariki alfajiri ya kuamkia Septemba 10, baada ya kugongwa na gari eneo la Maji ya Chai, Arusha wakati akivuka barabara kwenda nyumbani kwake jirani na eneo hilo saa 7 usiku.

Mwili wake utaagwa leo Ijumaa, nyumbani kwake Arusha na kusafirishwa kwenda kijijini kwao Nangwa, Katesh, ambako utazikwa kesho Jumamosi.

Akizungumzia dakika za mwisho za mumewe, Eva alisema saa chache kabla ya kufikwa na mauti, alimpigia simu.

"Tulikuwa tumekubaliana kwamba hatokuwa akichelewa kurudi nyumbani, siku hiyo akawa amekiuka makubaliano, nilipoona usiku unazidi, nikampigia alikuwa yupo na mjomba wake.

"Aliniambia anarudi, ila akaomba nimtumie nauli kwa kuwa pesa aliyokuwa nayo aliitumia, nilifanya vile, na alipokwenda kupanda gari ili kurudi nyumbani niliongea naye akaomba msamaha kwa kuchelewa, nikiwa bado namsubiri akanipigia simu," anasema.

Anasema, baadaye simu yake ikaita, alipoiangalia akaona jina la mume, akaipokea. Lakini aliyekuwa akizungumza kutokea upande wa pili hakuwa mumewe bali mtu mwingine aliyekataa kujitambulisha na kumpa taarifa kwamba mwenye simu amepata ajali na amefariki dunia.

"Sikuamini, nilienda eneo la tukio na kukuta kweli ni Gidabuday, mtu ambaye nilitoka kuzungumza naye muda mfupi tu uliokuwa umepita," anasema.

RIADHA ILIKUWA IKIMLIZA

Eva anasema, katika maisha yao ya ndoa, mumewe amekuwa katika maumivu makali ya moyo kila alipokuwa akikumbuka tukio la kuondoshwa kwenye riadha.

"Alipojiuzulu ukatibu mkuu wa RT, Gidabuday ni kama alipata msongo, tukio lile lilikuwa linamuumiza mno, kuna nyakati alikuwa akilia machozi kila alipolikumbuka, ameondoka akiteseka kuhusu riadha, aliipenda," anasema.

Gidabuday alijiuzulu nafasi ya katibu mkuu mwaka 2019, ikiwa imepita miaka mitatu tangu alipochaguliwa kuongoza shirikisho hilo Novemba 2016.

Kujiuzulu kwake kulitangazwa katika mkutano wa waandishi wa habari ulioongozwa na rais wa RT wa wakati huo, Anthony Mtaka, uliofanyika jijini Dar es Salaam huku mwenyewe akisisitiza uamuzi huo umetokana na maslahi mapana ya riadha nchini.

Akiwa mwenye huzuni, na akizungumza kwa upole tofauti na alivyozoeleka, Gidabuday katika mkutano huo alizungumza kwa ufupi sana kujiuzulu kwake nafasi ya katibu mkuu wa RT.

Mbali na kuwa katibu mkuu, amewahi kuwa miongoni mwa waasisi wa mbio ya Sokoine Marathon na hadi mauti inamkuta alikuwa ni Katibu wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ya RT.

WADAU WANAVYOMZUNGUMZIA

Rais wa RT, Silas Isangi anasema alimfahamu Gidabuday miaka mingi, akiwa ni bosi wake wakati huo yeye Isangi alikuwa ni mwenyekiti wa riadha Mwanza na Gidabuday akiwa katibu mkuu wa RT.

"Nimefanya naye kazi akiwa bosi wangu hadi alipomaliza muda wake, nilipokuwa Rais RT nilimpa nafasi kwenye Kamati ya Kabadiliko ya Katiba, alikuwa mchapakazi."

Anasema, alihitimisha jukumu hilo akiwa na kamati yote Agosti 24 na siku iliyofuatia alishiriki kumkabidhi yeye Isangi na Septemba 8, siku mbili kabla ya mauti alimpigia simu.

"Nilikuwa nipo Mahakamani, akaniambia Rais kuna jambo nataka nikwambie, nikamwambia tutazungumza baadaye, lakini hakuniambia hilo jambo, hadi mauti inamkuta," anasema Isangi.

Anasema familia ya riadha imeondokewa na mtu mchapakazi, ambaye kesho watamuaga kwa ajili ya kumsindikiza kwenye nyumba yake ya milele keshokutwa.

Chanzo: Mwanaspoti