Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkasa wa Lineker na unafiki wa wazungu

Gary Lineker Wazungu Garry Lineker

Wed, 15 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mara nyingi nchi zilizoendelea zimekuwa zikijigeuza askari wa kuchunga nchi nyingine kwa kila zinachofanya. Yaani hawa walioendelea hudhani wanaoendelea hawawezi kuwaza, hawawezi kufikiria na hawajui chochote.

Kupitia fimbo zao za haki za binadamu na demokrasia, nchi hizo zimekuwa zikizichapa nchi zinazoendelea zinavyotaka. Ikitokea kwenye nchi inayoendelea kuna mwanaharakati fulani kasema kitu ambacho hakikuifurahisha mamlaka na ikamchukulia hatua wao huja juu na kuhubiri kitu kinachoitwa uhuru wa kutoa maoni.

Wanasisitiza kabisa ni kwamba binadamu wana haki ya kupatiwa uhuru wa kutoa maoni katika nchi yao. Kuwanyima haki hiyo ni kukiuka haki za binadamu. Lakini sasa imekuwa kinyume, uhuru wa kutoa maoni umewekewa mipaka kwenye moja ya mataifa makubwa yanayopigania haki hiyo kwa nchi zinazoendelea.

Hali sio hali nchini Uingereza. Hali si hali kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Na hali si hali kwenye ulimwengu wa michezo nchini Uingereza. Hayo yanafuatia kitendo cha shirika la umma la BBC kumsimamisha kazi mtangazaji wake mwenye heshima kubwa nchini humo, Garry Lineker.

Lineker ni mmoja wa watu maarufu nchini Uingereza kwa sababu alikuwa nyota wa soka akichezea klabu za Leicester City, Tottenham Hotspur na Barcelona. Pia alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya England.

Akiwa na timu ya taifa, Lineker alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia 1986 - lile la Maradona akiwa katika ubora wake. Hata ile mechi ya bao la mkono wa mungu kati ya England na Argentina ambayo Maradona alifunga mabao mawili, moja la mkono na lingine la uwezo wa hali ya juu, Lineker alifunga bao moja na mechi kuisha 2-1.

Nyota huyo baada ya kustaafu soka aligeukia kwenye habari na akawa mtangazaji wa runinga mbalimbali nchini humo ikiwemo BBC na BT Sport kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiwa BBC, Lineker hutangaza kipindi maarufu na kikongwe cha Match of the day ambacho ni maalumu kwa ajili ya uchambuzi wa Ligi Kuu ya England.

Kipindi ni maarufu na kikongwe kwa sababu kilianza mwaka 1964. Lakini sasa BBC imeamua kumsimamisha kazi mtangazaji huyo kwa kosa la kutoa maoni mtandaoni. Jumanne, Machi 7, 2023, Lineker kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter alikosoa sera za serikali ya nchi hiyo kuhusu wahamiaji na uhamiaji haramu.

Serikali ya Uingereza chini ya Waziri Mkuu ‘mh amiaji’, Rishi Sunak imetunga sheria kali sana dhidi ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini humo kusaka maisha.

Sunak ni mwanasiasa mwenye asili ya India ambaye wazazi wake walihamia Uingereza wakitokea Afrika Mashariki. Baba yake alizaliwa Kenya na mama yake alizaliwa Tanzania. Lakini serikali yake imetunga sheria kali ya uhamiaji kuliko nchi yoyote duniani.

Katika sera hiyo, mhamiaji haramu akikamatwa anawekwa ndani na baadaye anasafirishwa kupelekwa Rwanda na anapigwa marufuku maisha yake yote kurudi nchini humo. Rwanda iliingia mkataba na Uingereza kwa ajili ya kambi ya watu wa aina hiyo.

Sera hii inapingwa vikali na umoja wa mataifa pamoja na mashirika ya haki za binadamu duniani.

Katika kukosoa kwake, Lineker aliifananisha sera hiyo na sera za manazi wa Ujerumani wakati wa Adolph Hitler. Ukosoaji huo ukawachefua wakuu kuanzia serikalini hadi BBC kwenyewe, na kumsimamisha kazi.

Lineker huwa na wachambuzi kama Alan Shearer ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu England na Ian Wright aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Arsenal, lakini rekodi yake ilikuja kuvunjwa na Thierry Henry.

Kusimamishwa kwa Lineker kukawakwaza wachambuzi wake nao wakasusa kuingia studio kama ishara ya kumuunga mkono mtangazaji wao. BBC wanasema Lineker kama mtangazaji wa michezo kwenye chombo cha umma hakupaswa kujihusisha na siasa.

Kauli hiyo ni moja ya hoja dhaifu zaidi kuwahi kutolewa kama utetezi kwa chombo kikubwa kama BBC. Kuelekea Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, Lineker aliruhusiswa na BBC kukosoa rekodi mbaya ya haki za binadamu za Qatar.

Nchi zilizoendelea hazikupenda Qatar kupewa haki ya kuandaa Kombe la Dunia na zilitumia kila silaha zilizokuwa nazo kuhakikisha zinawatoa waandaaji hao kwenye reli. Lineker aliru-husiwa kusema chochote cha kisiasa kuhusu Qatar na alionwa shujaa. Leo kasema kuhusu Uingereza kaonekana mbaya. Unafiki!

Chanzo: Mwanaspoti