Uongozi wa Yanga, umepiga hesabu kali na kubaini kuwa, tiketi yao ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika inaanzia katika mchezo ujao wa dhidi ya Real Bamako Mali.
Yanga kwa sasa wanakamata nafasi ya pili katika Kundi D la michuano hiyo wakiwa na pointi tatu sawa na TP Mazembe, huku vinara ni US Monastir wenye pointi 4, wakati Real Bamako wana moja.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Yanga tunahesabu zetu ambazo tayari tumeziweka kwenye michuano hii ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakati tukiwa tunaenda nchini Mali kucheza na Real Bamako, tumejiwekea malengo yetu.
“Tuna malengo ya kuhakikisha tukiwa ugenini tunafanikiwa kuondoka na pointi hata moja ama ushindi kabisa kwani hiyo itakuwa ni njia mojawapo ya sisi kupata nafasi nzuri zaidi ya kusonga mbele.
“Maana tukipata pointi moja ugenini, tutakuwa na michezo miwili ya nyumbani ambayo ni dhidi ya Real Bamako marudiano na US Monastir ambapo michezo hii kama tutashinda yote basi tutakuwa na uhakika wa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.”
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema: “Kila hatua ambayo tunashiriki ni kubwa na tunapambana kupata matokeo mazuri, malengo ni kuona tunafika robo fainali.
“Kufika hatua hiyo sio kazi nyepesi, ni lazima kila mmoja apambane kutimiza majukumu yake kwani hatua ambayo tupo kila mmoja anafanya kazi kubwa kutokana na ushindani uliopo.”