Wasauzi wanavyojadili goli lililokataliwa
Kama ilivyo kwa Tanzania, wapenzi wa mpira wa miguu wa Afrika Kusini wamekuwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii kama shuti la Stephen Aziz Ki lilizaa goli katika mechi baina ya Yanga na Mamelodi Sundowns jana Aprili 5, 2024 au halikuwa goli.
Baadhi wanaona lilikuwa goli halali, wengine wanaona uamuzi wa refa ulikuwa sahihi lakini wapo wanaoona refa pia aliinyima Sundown mkwaju wa penati na kushindwa kuwazawadia Yanga kadi nyekundu na hivyo mambo yalibalansi!
Ukurasa wa Facebook wa mwandishi wa habari za mchezo nchini humo, Lorenzo Kohler ambaye alirusha sehemu ya maelezo ya Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akidai Yanga imepokwa ushindi, ni moja ya sehemu ambazo zimezua mjadala mrefu unaoendelea hadi sasa.
Kwa mfano kuna huyu Kemmy Msweli anasema: "Mimi ni sapota mkubwa wa Sundowns lakini lile lilikuwa goli halali, lisilo na mushkeli wowote.. Sifurahishwi na timu yangu kushindwa kufunga goli la mapema ambalo lingeichanganya Yanga.
Lakini Menzi Dubazane anasema: "Yanga wanapiga kelele sana wakijua kabisa walifuzu kwa bahati tu hatua ya makundi... Ni nani huyu (Gamondi) wa kuhoji uadilifu wa soka la Afrika. Tunataka timu bora zinazofaa kuwa vinara wa soka la Afrika na kwa bahati mbaya Yanga sio miongoni mwao lakini tunawahimiza waendelee kujaribu."
Mtu mmoja anayejiita Spindoctor Mahyadi anamjibu Dubazane akisema: "Kama unadhani timu yako bora kwa nini mlihitaji usaidizi wa VAR ili kufuzu nusu fainali? Mlifunga hata goli la kuotea? Sundown sio timu kubwa, mnajishughulisha tu na bosi wenu kupanga matokeo."
Mwingine, Mbona Malaki amesema: "Mamelodi imethibitisha sio timu bora, sifa ziende kwa refa na VAR."
Huyu mwingine, Abhutii Amster anasema: "Huyu kocha (Gamondi) naye pia alinufaika na refa. Je, rafu aliyofanyiwa Mudau haikuwa kadi nyekundu? Na je, hakukuwa na penati kipindi cha kwanza?"
Mjadala ni mrefu. Huko kwenu mnajadili pia?