Mchambuzi maarufu wa masuala ya soka nchini, Amri Kiemba amesema kuwa Kocha wa Geita Gold, Hemmed Morocco sio mwalimu ambaye anakaa muda mrefu kwenye timu kwa sababu hapendi migogoro.
Mchezaji huyo wa zamani wa vilabu vya Simba, Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania amesema Mzanzibar huyo ni kocha mzuri na anapenda kuishi kirafiki na wachezaji wake hivyo iwapo Geita watamtumia vizuri basi atawafikisha mbali.
"Nimefundishwa na makocha wengi wa ndani na nje ya nchi, Hemmed Morocco ni miongoni mwa makocha walionifundisha, ni kocha ambaye kama wachezaji wataweza kushika yale ambayo anaekeleza kwenye uwanja wa mazoezi Geita inaweza kufanya makubwa.
"Morocco ni kocha mzuri lakini pia anajua kuishi na wachezaji, mtu anahisi anawajibu wa kumpambania kocha kutokana na namna ambavyo kocha anampa heshima na upendo.
"Ni kocha ambaye mara nyingi humuoni akikaa muda mrefu kwenye timu kwa sababu ikianza mizozo anaweka begi lake begani anarudi nyumbani Unguja," amesema Amri Kiemba.