Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mivutano ya kisiasa na soka Uarabuni

Edouard Mendy Cmp Mivutano ya kisiasa na soka Uarabuni

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siasa ni neno lenye asili ya kiarabu ambalo maana yake ni 'Usimamizi wa Mambo ya Kijamii'.

Kiswahili kimelichukua neno hili kama kilivyoyachukua maneno mengine mengi kutoka lugha ya kiarabu, kama neno dini. Kwa kiarabu, dini maana yake ni utaratibu wa maisha ya mwanadamu.

Maneno haya mawili unaweza ukayachukulia kawaida sana kwa nchi kama Tanzania ambako utengamano wa kijamii (social stability) ni mkubwa sana.

Lakini huko kwenye asili ya maneno haya mawili, hali siyo ya kawaida hata kidogo. Utengamano wa kijamii katika nchi za kiarabu ni wa mashaka tangu zama za manabii.

Ndiyo maana kuna msemo maarufu wa kiarabu unaosema, Eshteri al-jar qabl ed’dar (Mnunue kwanza jirani kabla hujanunua nyumba).

Neno Dar unaloliona mwisho hapo maana yake ni nyumba... Ed'dar ni sawa na kusema The House... ila Kiswahili hakina tafsiri ya The.

Hapo kwenye Dar ndipo inapotokea Dar ya kwenye Dar es Salaam. Dar maana yake ni nyumba, ni neno la kiarabu. Dar Es Salaam asili yake ni Dar-ul-Salaam ambayo maana yake ni nyuma iliyo salama.

Kwa hiyo waarabu wanaposema mnunue kwanza jirani kabla hujanunua nyumba, maana yake chagua jirani mwema kwanza kabla hujachagua nyumba nzuri ya kuishi.

Jirani mbaya anaweza kuwa mikosi, na jirani mwema ni baraka. Waarabu wamekuja na misemo yote hii kwa sababu ya historia yao ya misukosuko katika eneo lao.

Eneo hilo kongwe linalotajwa kwenye vitabu vyote vya dini za Ibrahim, limekuwa likikumbwa na misukosuko ya kisiasa na kidini miaka na mikaka.

Miongoni mwa nchi zinazoishi kwa mashaka ya mahusiano ya kisiasa na kidini ni Iran na Saudi Arabia.

Haya ndiyo mataifa makubwa zaidi katika ukanda huo lakini tofauti zao za kidini na kisiasa zimewafanya waishi maisha ya gano la kisigino cha mguu wa binadamu na kichwa cha nyoka.

Kisigino kinatakiwa kikanyage kichwa cha nyoka wakati wowote, na nyoka anatakiwa ang'ate kisigino wakati wowote...atakayezubaa imekula kwake.

Jumatatu ya Oktoba pili mwaka huu, mahusiano ya mataifa haya yaliingia kwenye sura nyingine upande wa michezo.

Timu mbili za kutoka mataifa haya zilitakiwa zicheze mechi ya mashindano ya ligi ya mabingwa Asia.

Al Ittihad ya Saudi Arabia, timu iliyojaa nyota waliotamba Ulaya kama Karim Benzema, N'Golo Kante na Fabinho, ilisafiri hadi mjini Isfahan nchini Iran kucheza na timu ya Sepahan.

Watazamaji zaidi ya 60,000 wakiwa ndani ya dimba la Naghsh-e Jahn kusubiri kipute kianze, ikaja taarifa kwamba wachezaji wa Al Ittihad wamegoma kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa sababu za kisiasa.

Ndani ya uwanja uliokuwa utumike kulikuwa na sanamu za Qasim Soleiman, kamanda wa kijeshi wa Iran aliyeuawa na majeshi ya Marekani mwaka 2020 nchini Iraq.

Mwaka 2018 Saudi Arabia ilimuweka kamanda huo kwenye orodha ya magaidi hatari wanaosakwa kwa udi na uvumba.

Nchini Iran, Qasim Soleiman ni shujaa wa taifa, nchini Saudi Arabia, Qasim Soleiman ni gaidi hatari.

Kama timu ya Saudi Arabia, Al Ittihad haikuwa na namna nyingine zaidi ya kugoma kutoka vyumbani hadi sanamu la Qasim Soleiman litolewe.

Na wenyeji wakakaza kwamba sanamu la shujaa wao haliwezi kutolewa. Hali ikawa hivyo hadi mechi hiyo ikafutwa.

Mivutano ya kisiasa na kidini ya Iran na Saudi Arabia imeathiri sana soka ambapo tangu 2016 mechi baina ya timu za kutoka nchi hizi mbili zimekuwa zikifanyika katika uwanja huru, yaani katika nchi nyingine.

Ni Septemba ya mwaka huu tu ndiyo timu zikaanza kuruhusiwa kucheza ndani ya nchi hizo, lakini sasa tayari matatizo yameshaanza.

Chagua jirani mwema kwanza kabla hujachagua nyumba nzuri ya kuishi, bahati mbaya sana kwenye siasa za kimataifa huwezi kuchagua jirani.

Saudi Arabia na Iran ni majirani lakini tofauti zao za kisiasa na kidini zimewagawa kiasi kwamba hadi michezo inaathirika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live