Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miujiza ya jezi ya Mayele, Simba hawaitaki watoa sababu

Mayele Kirumba 2022 Yannick Bangala na Fiston Mayele

Sun, 27 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati mastaa wengi wa miaka ya karibuni wakiikwepa jezi namba tisa kwa timu za Simba na Yanga, straika wa Yanga, Fiston Mayele amevunja mfupa uliowashinda wengi.

Katika kikosi cha Yanga, jezi namba 9 ilipewa jina la ‘Jezi ya Moto’ na anayeivaa lazima msimu uwe mbaya kwake na ataondoka tu. Ndani ya kikosi cha Simba haitumiki kabisa. Hakuna mchezaji anayeitaka. Kwa Mayele ambaye ni msimu wake wa kwanza Yanga imekuwa tofauti kwa sababu tayari ameifungia timu yake mabao 10 kwenye michezo 18 waliyocheza Ligi Kuu Bara akiwa ametupia jezi namba 9.

Mayele ametaja siri ya kuvaa jezi hiyo kuwa ni kutokana na kupoteza dada yake kwenye familia ambayo walizaliwa 10 na sasa wamebaki tisa.

“Mwanzo nilikuwa navaa jezi namba 10 kutokana na idadi ya watoto tuliozaliwa ndani ya familia, lakini baada ya kuondokewa na dada yangu na kubaki tisa nikaamua kubadili namba ambayo ndio naitumia hadi sasa,” anasema.

“Sina imani na utaratibu uliopita ndani ya Yanga kwamba namba tisa ina mkosi, kwa sababu naamini katika uwezo kwani namba na uwezo haviingiliani. Mbona navaa naanza kikosi cha kwanza na nafunga.”

Mayele anasema kujituma na kuamini katika kipaji ndio siri ya mchezaji kufanya vizuri, lakini suala la namba halina uhusiano wowote kwa sababu kuna wachezaji wanavaa kwa kupendezwa na uwezo wa mchezaji mkubwa anayevaa jezi hiyo.

Kiutamaduni, jezi namba tisa inahusika na ufungaji mabao, ingawa soka la kisasa mambo yamebadilika kidogo katika mbinu lakini kazi ya namba tisa inabaki ileile ya kucheka na nyavu.

Katika kikosi cha Simba, jezi namba 9 imefungiwa kabisa kabatini na hakuna mchezaji anayeivaa wala anayetaka hata kuisikia, kwani kila anayekuja kwenye timu anaikataa. Mwanaspoti linakuletea mastaa waliofanya vizuri na namba hiyo sambamba na walioshindwa kutamba nayo na kujikuta wakisepa kwenye klabu hizo.

ZAMOYONI MOGELA - SIMBA

Anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kuwahi kutokea aliyecheza timu zote mbili, lakini Simba ndiko kacheza kwa mafanikio makubwa kutokana na kucheza misimu mingi, huku Yanga akiitumikia msimu mmoja na kuamua kutundika daluga.

“Imani tu ndio zinawaharibu wachezaji, mimi nimecheza Simba kwa mafanikio na jezi hiyohiyo namba tisa na nilikuwa nafunga sana. Nakumbuka nilikuta inavaliwa na mtu sikumbuki nani, lakini kutokana na umahiri wangu wa kufunga nikapewa tisa,” anasena na kuongeza kuwa, “sina kumbukumbu nilifunga mabao mangapi ila nilikuwa imara sana eneo hilo.”

MAKUMBI JUMA - YANGA

Ni miongoni mwa washambuliaji hatari waliowahi kupita Yanga na kupachikwa jina la utani ‘Homa ya Jiji’ kutokana na umahiri wake wa kuzifumania nyavu.

Mkongwe huyo anasema: “Miaka tuliyokuwa tunacheza sisi tulikuwa tunavaa jezi kulingana na nafasi - namba tisa ilikuwa maalumu kwa ajili ya mshambuliaji, ukivaa lazima ujue kucheka na nyavu, nadhani miaka ya sasa wanachagua ilimradi na anayekataa kwa kusema ina gundu siwezi kumuelewa.

“Nilivaa namba tisa kipindi hicho nakumbuka kwa wiki nilikuwa nafunga mabao matatu hadi manne, kwa nini iwe na gundu? Wachezaji wa sasa hawajitambui wewe u’shawahi kuona wapi fundi anachagua hadi kiatu cha kuvaa? Ukijua unajua kwa chochote unafanya bila kuwa na machaguo.”

EDWARD CHUMILA - SIMBA

Aliingia Simba kuziba nafasi ya Mogela baada ya kupata nafasi ya kwenda Uarabuni kucheza soka la kulipwa na alikabidhiwa jezi namba tisa na kugeuka kuwa kipenzi cha wana Msimbazi kutokana na kuwafunga watani zao Yanga mara kwa mara.

BONIFACE AMBANI

Mkenya huyu alisajiliwa na Yanga kutoka Sporting Club de Goa ya India na alianza kuvaa namba 9 na baadaye alihamia 24 ambapo aliisaidia timu hiyo kupata mafanikio kwa kutwaa mataji mengi na msimu wa 2008/9 aliibuka mfungaji bora akiwa na maba 18. “Ni jezi ambayo ina majukumu makubwa sana uwanjani, ukivaa unaonekana ni mchezaji muhimu kikosini kwa sababu inahusishwa na ufungaji wa mabao. Imekuwa ikikimbiwa kwa sasa kwa sababu washambuliaji wengi wa sasa hawajitambui,” anasema.

“Miaka yetu huwezi ukavaa jezi hiyo ukamaliza dakika 90 bila kufunga, kwa sasa mchezaji anavaa na hana maajabu uwanjani. Ndio maana wanaikwepa. Hawataki kuonekana kana kwamba hawaitendei haki hiyo jezi, ndio maana wanaikwepa.”

MOHAMMED HUSSEIN ‘MMACHINGA’ - YANGA

Ni mshambuliaji ambaye amecheza kwa mafanikio Yanga na kua-cha rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa ya kupachika mabao 26 ndani ya msimu mmoja na baadaye alihamia Simba.

Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anasema tatizo lililopo kuhusu jezi hiyo ni imani tu, lakini alipokuwa anacheza Yanga aliacha kuvaa namba 10 akavaa namba 9 na kupata mafanikio.

“Hizo zote ni imani tu. watu wana matatizo wenyewe, kama mshambuliaji anakaa mbali na goli au hana wapishi wazuri wa kumtengenezea nafasi, hataweza kufunga,” anasema.

MRISHO NGASSA-YANGA

Ngassa aliyepewa jezi hiyo aliporudi Yanga akitokea Simba aliivaa katika mechi za awali dhidi ya Kano Pillars ya Nigeria ambapo hakuonyesha kiwango kama alivyokuwa amezoeleka na baadaye aliigomea akapewa namba 17 anayoivaa hadi sasa.

Ngassa alirejea Yanga wa-kati ambao jezi namba nane ilikuwa inavaliwa na Haruna Niyonzima ambaye aligoma kuiachia.

Akiwa Azam FC alikuwa anavaa jezi namba 16 na aliendelea kuivaa hata alipohamia Simba SC ambako mwishoni akawa anavaa namba nane, lakini aliporejea Yanga SC alikuta namba 16 anavaa Nizar Khalfan, ambaye naye aligoma kuiachia.

OMEGA SEMA - YANGA

Ndiye aliyekuwa anaitumia jezi namba tisa baada ya kuondoka kutokana na kukosa namba ya kucheza kikosi cha kwanza akiishia kusota benchi na uongozi wa timu ulimtoa kwa mkopo Tanzania Prisons ya Mbeya.

RELIANTS LUSAJO - YANGA

Alijiunga na Yanga 2013 akitokea masomoni na baada ya kutua tu alipewa namba 9 ambayo alidumu nayo hadi alipoondoka kikosini. “Sina kumbukumbu nzuri nadhani nilifunga mabao mawili tu kwa sababu nilikuwa nacheza nafasi ya kiungo tofauti na sasa ambapo nacheza nafasi ya ushambuliaji.

“Tangu nilipokuwa mdogo nilipenda namba tisa, ni namba ambayo nilikuwa naipenda sana zamani kipindi mdogo kwa sababu ya Ronaldo de Lima na ndio maana nilipofika Yanga nilioba namba hiyo.”

GENILSON SANTOS ‘JAJA’ - YANGA

Alianza vizuri akiiongoza Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani walipoifunga Azam 3-2 na yeye akipachika mabao mawili, lakini baadaye mpira ulimshinda. Jaja aliaga kwenda mapumziko nchini kwao hakurudi tena na soka lake Yanga liliishia hapo.

KPAH SHERMAN - YANGA

Sherman alijiunga na Yanga Desemba 2014 akitokea Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus na aliichezea Yanga mara 27 na kuifungia mabao sita.

Pamoja na Yanga kushindwa kunufaika na ubora wake uwanjani walimuuza Mpumalanga Black Aces ‘AmaZayoni’ ya Sauzi

PATRICK SIBOMANA - YANGA

Ilikuwa Agosti 3, 2020 uongozi wa Yanga ulitangaza majina saba na Sibomana aliyekuwa akivaa jezi hiyo kabla ya kuhamia namba 11 (picha kubwa), kuwa miongoni mwa waliovunjiwa mikataba kutokana na kushindwa kuonyesha uwezo. Wengine walikuwa Ali Mtoni (marehemu), Ali Ali, Yikpe Gislain, Eric Kabamba, Rafael Daudi na Issa Maundu. Sibomana aliondoka akiwa amefunga mara tano na kutoa pasi tatu.

SADNEY URIKHOB -SIMBA, YANGA

Mwaka 2019, Simba wakifanya maandalizi ya msimu walicheza Kombe la SportPesa na walimleta nchini straika Sadney Urikhob kutokaa Namibia aliyeshindwa kufanya vizuri.

Akiwa Simba, Urikhob kwa majaribio baadhi ya me-chi ali-kuvaa namba tisa, ila m-wi-sho wa siku hakufanya vizuri na ku-shi-ndwa kusajiliwa.

Ba-ada Urikhob kushindwa kusajiliwa na Simba aliibukia Yanga alikosajiliwa miaka miwili ila hakufanya vizuri na kutumikia mwaka mmoja.

WILKER DA SILVA - SIMBA

Mwaka 2019, Simba waliwasajili Wabrazili watatu akiwemo straika Wilker da Silva aliyedumu kwa msimu mmoja tu baada ya kushindwa kufanya vizuri.

Da Silva aliyekuwa anavaa jezi namba tisa hakupata muda wa kutosha kucheza kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

BETRAM MWOMBEKI -SIMBA

Mwaka 2013, Betram Mwombeki baada ya kutua katika kikosi cha Simba kutokea Marekani alikuwa akivaa jezi namba tisa ila ghafla alibadilisha na kuvaa 23.

HENRY JOSEPH - SIMBA

Mwaka 2013 baada ya kurejea nchini kutoka Norway alikokuwa anacheza soka nahodha wa zamani Simba, Henry Joseph alijiunga na timu yake na alitakiwa kuvaa namba tisa.

Joseph aliwaambia viongozi Simba hakuwa tayari kuvaa jezi hiyo kutokana na mambo mawili.

“Kwanza niliwaambia wakati naondoka Simba nilikuwa navaa jezi namba sita na ndio chaguo langu, kama hiyo inavaliwa na mchezaji mwingine na hayupo tayari kuniachia basi nitafanya chaguo lingine,” anasema Joseph.

“Nikawaambia wanipe jezi kati ya namba 12 au 14 naweza kuvaa, lakini hiyo namba tisa siyo chaguo langu na wala hainivutii kuvaa, lakini mastraika ndio wakivaa inakuwa sawa, tulikubaliana na nikaiacha.”

GERVAS KAGO - SIMBA

Jezi namba tisa mwaka 2011 alikuwa akivaa Gervas Kago aliyesajiliwa kutoka Jamhuri ya Kati na maisha yake kikosini hayakuwa katika kiwango bora.

BLAGNON/MAVUGO - SIMBA

Baada ya kuwasili nchini 2016 kumalizana na Simba, mshambuliaji raia wa Burundi, Laudit Mavugo aliomba jezi namba tisa. Wakati huo ilikuwa inavaliwa na Blagnon Frederick kutoka Ivory Coast ambaye Simba ilimtoa African Sports ya Abidjan.

Mavugo na Blaignon wote walishindwa kufanya vizuri.

AMIS TAMBWE - SIMBA

Kuhusu jezi namba tisa, Tambwe anasema wakati anatua Simba alisikia mastaa waliovaa jezi walishindwa kutamba. Lakini, upande wake haikumtisha kwani aliamini anayeivaa anaweza kufanya mambo makubwa.

Licha ya kutoamini hilo, hakuwa tayari kuvaa jezi hiyo kwa sababu aliamini jezi namba 17 ilimpendeza baada ya kutua Msimbazi 2013 akitokea Vital’o ya Burundi na alicheza msimu mmoja tu na kufanikiwa kupachika mabao 19 na kuibuka mfungaji bora wa msimu na baada ya mkataba wake kwisha alimtemwa na kutua zake Yanga.

MAMENEJA

Akizungumzia jezi namba tisa, mchezaji wa zamani wa Toto Africa, Kagera Sugar na Azam FC, Philip Alando anasema hakuna uhusiano wowote kati ya namba ya jezi na uwezo wa mchezaji uwanjani na kuthibitisha kuwa ni utashi unaowafanya wachezaji wengi kuamini katika namba.

“Kulikuwa na taarifa kwamba jezi namba 10 inavaliwa na mastaa wa timu, kitu ambacho kiliwajengea wachezaji wengi kuamini hivyo na kutaka kuivaa, lakini kuna mastaa wengi wamecheza vizuri na hawajawahi kuivaa mfano Mrisho Ngassa kacheza kwa mafanikio na amepita timu tatu kubwa Ligi Kuu hajawahi kuivaa,” anasema Alando.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu anasema wachezaji wamekuwa wakiamini katika bahati. “Nimekutana na mastaa wengi wanasema wana bahati na namba fulani na wengine ni mapenzi kutokana na kuona imevaliwa na wachezaji wanaowapenda,” anasema Rweyemamu.

Wakati ikiwa hivyo katika timu hizo kubwa Ligi Kuu Bara, huko England namba tisa pia ina mambo yako. Cheki mastaa waliobamba na kutoitendea haki.

MANCHESTER CITY

Kwenye kikosi cha Man City namba tisa inavaliwa na Mbrazil Gabriel Jesus aliyecheza mechi 20 na kufunga mabao mawili na pasi za mwisho saba.

LIVERPOOL

Namba tisa inavaliwa na Roberto Firmino aliyecheza mechi 16 msimu huu na kufunga mabao matano na kutoa sisti tatu. Mwingine aliyetumia jezi hiyo alikuwa Fernando Torres 2007–11 alicheza mechi 102 na kufunga mabao 65.

CHELSEA

Msimu huu Romelu Lukaku anavaa namba tisa na amecheza mechi 19 za ligi, akifunga mabao matano hana pasi ya mwisho.

Wachezaji wengine waliowahi kuivaa Chalsea na kushindwa kufanya vizuri ni Fernando Torres aliyecheza mechi 110 na kufunga mabao 20, Hernan Crespo 2003-08 mechi 49 na kufunga mara 20.

ARSENAL

Jezi hiyo inavaliwa na Mfaransa Alexandre Lacazette aliyecheza mechi 23 za ligi ametoa pasi za mwisho saba na kufunga mabao manne msimu huu.

TOTTENHAM HOTSPUR

Katika kikosi cha Spurs hakuna anayevaa jezi hiyo kwa sasa. Hata hivyo, 2008-12 ilivaliwa na Roman Pavlyuchenko katika mechi 78 alifunga mabao 20. Dimitar Berbatov (2006-08) mechi 70 na kufunga mabao 27.

MANCHESTER UNITED

Kwa sasa hakuna anayevaa namba tisa tangu ilipoachwa na Anthony Martial dirisha dogo la usajili Januari, mwaka huu. Martial yupo Sevilla kwa mkopo, lakini akiwa na Man United alicheza mechi 175 na kufunga mabao 56. Hata hivyo, kuanzia 2008–12 jezi hiyo ilitumiwa na Berbatov na katika mechi 108 alifunga mabao 48.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz