Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mitatu ya Samia, michezo imenoga

Mitatu Ya Samia Mitatu ya Samia, michezo imenoga

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

“Moja ya nyakati ambazo nitazikumbuka kwa muda mrefu katika utumishi wangu kwenye michezo ni Aprili 4, 2017.

Nina sababu nyingi za kuikumbuka siku hiyo ambayo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika nyumbani kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kuketi naye kwenye meza ya chakula alichokiandaa.

Kwangu mimi mambo ya kukumbuka zaidi yalikuwa mawili; moja nilivutiwa kumwona Makamu wa Rais kwa upole akiwakaribisha mezani na kuwapakulia chakula vijana wa timu ya taifa ya soka ya umri chini ya miaka 17 waliokwenda kumuaga wakielekea kambini Morocco wakiwa njiani kwenda kwenye Fainali za Afrika kwa vijana (Afcon U-17) za Gabon.

La pili ni tukio la kusikitisha la kuzuiliwa na madalali wa mamlaka ya mapato kwa basi lililokuwa linawapeleka vijana wa Serengeti Boys kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Makamu wa Rais kuwaaga vijana hao katika kilichodaiwa shirikisho lilikuwa na deni la kodi.

Pamoja na nasaha alizowapa vijana, Makamu wa Rais alizielekeza mamlaka husika kutumia busara katika kudai mapato na hivyo kesho yake basi hilo liliachiliwa.

Matukio hayo nayakumbuka kama vile jana, pia nikiongea na baadhi ya vijana hao, ambao kwa sasa ndio wanatengeneza uti wa mgongo wa timu ya taifa ya wakubwa (Taifa Stars), bado wanaikumbuka siku hiyo.

Ni nukuu kutoka makala yangu ya kwanza katika safu hii, yaliyokuwa na kichwa cha habari ‘Tanzania chini ya Samia ina fursa tele kwa uwekezaji katika michezo’.

Wakati naandika makala niliyoyataja hapo juu, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa hana muda mrefu ndani ya Ikulu.

Hata hivyo, dalili zilikuwa wazi alikuwa ni kiongozi ambaye angekuja kufanya makubwa au tuseme mazuri katika ustawi na maendeleo ya michezo kwa faida ya familia ya michezo na taifa kwa jumla.

Rekodi yake ya kuunga mkono michezo, hasa ile ya wanawake na vijana, awali akiwa makamu wa rais ilikuwa ni dalili tosha michezo kama sekta imepata wakati sahihi wa kuneemeka. Niliweka wazi kama Dk Samia angejishughulisha na mambo ya michezo kwa vijana, ushiriki kimataifa, kuandaa mashindano ya kimataifa, kuangalia muundo wa wizara na juu ya yote kuwa na utashi wa kisiasa, basi michezo itaweza kusonga mbele.

Makala 77 zimeshapita tangu wakati huo na Rais Samia anazidi kudhihirisha mapenzi na mwelekeo wake katika sekta ya michezo.

Michezo ni sekta muhimu sana katika maendeleo na ustawi wa nchi. Michezo ni uchumi, michezo ni ajira, michezo ni afya, michezo ni furaha.

Michezo ni nyenzo ya kuleta amani na umoja ndani ya nchi, pia ni nyenzo ya diplomasia. Kwa kiongozi wa taifa anayetambua jukumu lake, michezo ni moja ya vitendea kazi vyake katika kufanikisha makusudi yake ya kijamii, kiuchumi na hata ya kiusalama na kidipkomasia.

Hata hivyo, nyenzo hiyo hupata nguvu zaidi inapopata kiongozi ambaye pamoja na kuitumia pia ana mapenzi nayo.

Rais Samia katika miaka yake mitatu madarakani ameweza kuitumia vizuri nyenzo hii na kwa kweli mwelekeo wa mbele unatoa taswira ya matumaini. Mapenzi yake kwa michezo yanaonekana dhahiri.

Tangu ameingia madarakani, Rais Samia amekuwa na msisitizo wa kuanzisha programu za michezo ya vijana mitaani na katika taasisi za umma kama Shule za Msingi na Sekondari. Shule za Sekondari za mwelekeo wa michezo zimekwishaainishwa karibu kwa kila wilaya japo bado hazijaimarishwa kwa upande wa miundombinu, vifaa na walimu wa taaluma ya michezo.

Pia hivi karibuni serikali kupitia Tamisemi imetangaza kuongezeka kwa mchepuo wa michezo katika masomo ya juu ya Sekondari yaani kidato cha tano na sita.

Vituo binafsi vya kukuzia vipaji au maarufu kama akademi vimepewa uhuru wa kuendesha shughuli zao za kukuza vipaji na vingine sasa vinashirikiana na vituo vya nje na hata vilabu vya michezo vya kimataifa jambo linaloleta matumaini.

Ushiriki wa Tanzania katika michezo mbalimbali kimataifa umeongezeka na kuna dalili ya timu zetu kuja kufanya vizuri.

Medali zimeanza kupatikana katika masumbwi, riadha na kuogelea hasa katika kiwango cha Afrika na Michezo ya Madola. Bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili timu zetu ziweze kushiriki Olimpiki na mashindano ya dunia kwa mafanikio.

Upande wa soka ambao kiukweli ndio mchezo wenye wafuasi wengi nchini, mchango wa Rais Samia unaonekana. Timu za taifa za vijana, wanawake na wakubwa zimeungwa mkono na serikali kwa kiwango cha juu. Kwa kweli katika uzoefu wangu, sikumbuki kipindi au utawala ulioweka mazingira mazuri ya kuendesha mpira kama utawala wa Samia. Mtihani unabaki kwa wanaozisimamia timu hizo za taifa kuhakikisha zinaendeshwa kwa mipango iliyothabiti ili kuwa na mafanikio endelevu.

Upande wa klabu za mpira wa miguu na ushiriki wake kimataifa nako hakuna swali. Tangu mwaka jana wakati klabu za Simba na Yanga zikicheza kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Komeb la Shirikisho mtawalia, Rais Samia alianzisha fungu maalum la fedha maarufu kama Goli la Mama na kutoa kiasi cha Sh5 milioni kwa kila goli na hata baadae alipandisha hadi milioni 10 kwa kadri mashindano yalivyosonga mbele. Haishangazi kuona msimu huu klabu hizo mbili zikisonga mbele na sasa ziko katika robo fainali ya Ligi ya Mbingwa wa Afrika, huku Tanzania ikiwa nchi ya pekee kuingiza timu mbili katika hatua ya robo fainali.

Mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alionyesha nia ya kuifanya Tanzania kuwa mmoja wa waandaaji wa michezo kimataifa. Alijitolea kuwa mlezi kwa kutoa fedha ya ufadhili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwa upande wa wanawake na sasa ufadhili huo umehamishiwa katika mashindano ya Challenge ya wanawake. Anakuwa kiongozi wa pili kufadhili mashindano ya Cecafa baada ya Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Ni kutokana na juhudi hizi sasa na Rais Mzee Yoweri Museveni wa Uganda amejitosa kudhamini Challenge Cup ya wanaume.

Juhudi za Rais Samia kwa kushirikiana na viongozi wa Kenya na Uganda zimefanikisha Afrika ya Mashariki kupewa uenyeji wa mashindano ya mataifa ya Afrika kwa soka maarufu kama Afcon 2027.

Ni jambo kubwa na lililohitaji nguvu na utashi wa kisiasa wa kiwango cha mkuu wa nchi kuweza kulifanikisha, matumaini ni makubwa mashindano haya yatakapomalizika yataacha alama kubwa kijamii, kimichezo, miundombinu na sekta nyingine za ukarimu na maendeleo kwa jumla.

Kazi yake kama Rais imekwishafanyika na kuonekana, mafanikio au mkwamo wa Afcon 2027 sasa yako mikononi mwa watendaji.

Pamoja na faida za kuandaa mashindano mengi, bado kuna gharama ya kuandaa miundombinu ya kufanyia michezo husika. Katika kauli zake mbalimbali Rais Samia ameonyesha utashi wa kuongeza miundombinu ya michezo na sanaa ya umma, lakini ameunga mkono uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya michezo. Moja ya hatua ambazo serikali imechukua ni kuondoa kodi kwenye vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya michezo kama vile nyasi bandia ili kuleta nafuu katika gharama za ujenzi. Viwanja kadhaa vya michezo vinategemewa kukarabatiwa, huku pia viwanja vipya vikijengwa kabla ya Afcon 2027 katika miji ya Arusha na Dodoma.

Miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ni injini mpya katika maendeleo ya sekta ya michezo.

Kuna changamoto kadhaa ambazo ni muhimu zikaangaliwa au zikatiwa chachu ili kuweza kufanya vizuri zaidi. Umuhimu wa kuangalia muundo wa wizara inayohusika na michezo kwani inaweza kufanya vizuri zaidi ikiunganishwa na wizara ya utalii.

Bajeti ya maendeleo ya michezo kupitia wizara ya michezo na ile ya Tamisemi inahitaji kuongezeka ili kusukuma mbele programu za vijana, mafunzo, vifaa na miundombinu.

Kwa mapenzi, nia na hatua anazochukua, ni matumaini ya safu hii kuwa tukijaliwa uzima mwakani wakati tunasherekea miaka 4 ya Rais Samia ofisini, mengi yatakuwa yametokea katika sekta ya michezo na Tanzania itakuwa katika viwango vya juu katika maendeleo ya michezo ikiwa watendaji wataakisi mtazamo na nia ya Rais Dr Samia Suluhu Hassan.

Chanzo: Mwanaspoti