Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miquissone afuzu mtihani wa Robertinho

Miquissone Simba Miquissone afuzu mtihani wa Robertinho

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' amefichua kuwa kwa sasa winga wake Luis Miquissone amepata ufiti ambao hakuwa nao mwanzoni na kuna uwezekano mkubwa akamtumia kwa dakika nyingi katika mchezo dhidi ya Al Ahly, Ijumaa hii katika Uwanja wa Benajmin Mkapa.

Katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu, Miquissone amecheza kwa dakika 180 tu ikiwa ni wastani wa dakika 36 tu huku akikosa mchezo mmoja, akicheza mmoja tu kwa dakika 90 na mingine mitatu akiingia kutokea benchi.

Sababu ambayo ilikuwa ikitolewa na Robertinho kwa kutomtumia kwa dakika nyingi winga huyo ni kutokuwa na ufiti, changamoto ambayo Robertinho ametamba kuwa Miquissone ameshaifanyia kazi na anaamini kuanzia mchezo dhidi ya Al Ahly, winga huyo atapata muda wa kutosha wa kucheza.

"Amekuwa na maendeleo mazuri sana (Miquissone). Wakati anafika na sasa kuna tofauti kubwa na jambo zuri ni kwamba yeye mwenyewe amekuwa na juhudi kubwa za kubadilika na anajituma sana.

"Kwenye mechi nyingi amekuwa akiingia kipindi cha pili lakini kwa nilivyomuona sasa, nafikiria kuanza kumpa nafasi ya kuanza kwenye mechi zetu zijazo ili tuone kama ataweza kuwa bora zaidi," alisema Robertinho.

Robertinho alisema anafurahia kuona Miquissone anaonyesha kiwango bora katika kipindi ambacho yeye na benchi lake la ufundi wanahitaji mchango wake kikosini.

"Mimi nimecheza nafasi ya winga miaka ya nyuma na nilikuwa natumia miguu yote lakini Miquissone ana hatari kubwa kwa kuwa na ubora wa kutumia vyema miguu yote. Kuna wakati mechi kubwa kama hizi (dhidi ya Al Ahly) zinaamriwa na wachezaji waliokomaa kama yeye.

"Ukiangalia muda tunaompa, umemuimarisha na akiwa sawasawa zaidi ya hapa kuna faida kubwa ataongeza kwenye safu yetu kule mbele," alisema Robertinho.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema anaamini Miquissone atapata muda mwingi wa kucheza dhidi ya Al Ahly ingawa mwenye uamuzi wa mwisho anabakia kuwa Robertinho.

"Uhitaji wa kocha utaamua lakini ile ni mechi kubwa ambayo kipaumbele cha kocha huwa ni wachezaji wenye uzoefu na Miquissone ana uzoefu," alisema Julio.

Beki wa zamani wa Simba, George Masatu alisema kinachomgharimu Miquissone ni uzito tu lakini ni mchezaji mwenye kipaji.

"Watu wanatakiwa kuelewa kwamba mpira una mambo mengi na kinachomgharimu Luis kwa sasa ni kuongezeka kwa mwili kunakomfanya ashindwe kukimbia kama zamani.

"Lakini naamini akipunguza vyakula anavyotumia atawashangazawengi. Nikimuangalia ni yuleyule kasoro uzito wake tu," alisema Masatu.

Chanzo: Mwanaspoti