Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miquissone, Kagere wamtibulia Gomes

Outplay Ed 0 Miquissone, Kagere wamtibulia Gomes

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Simba ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa Kundi A katika michuano hiyo ikiwa na pointi 10 ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri yenye alama saba, Jumamosi itaikaribisha AS Vita ya DR Congo yenye pointi nne katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mechi hiyo, Simba itakuwa ikihitaji sare tu ili kufuzu hatua ya robo fainali, wakati AS Vita yenyewe ikihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi ya kufuzu hatua hiyo, wakati huu Al Ahly ambao watakuwa ugenini dhidi ya vibonde wa kundi hilo, Al-Merrikh ya Sudan yenye alama moja, nayo ikihitaji ushindi huku ikiombea Wekundu wa Msimbazi hao washinde ili nao wakate tiketi kabla ya mchezo wa mwisho.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema anawakosa mapema katika maandalizi nyota hao wawili, Miquissone na Kagere, ambao jana walikuwa wakimalizia majukumu yao na timu za taifa kwenye mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Hivyo, Gomes ametuma ujumbe akiwataka Miquissone na Kagere kuhakikisha ifikapo kesho, Alhamisi wawe wameungana na wenzao kambini ikiwa ni siku mbili kabla ya kuivaa AS Vita.

Miquissone yupo na timu ya Taifa ya Msumbiji ambayo jana ilikuwa ikiikaribisha Cape Verde wakati  Kagere yeye alikuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda nchini Cameroon wakivaana na wenyeji hao.

Gomes alisema wako makini katika kuhakikisha wanafanyia kazi kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika mechi zilizopita, lakini kukiandaa kikosi chake kulingana na ubora wa AS Vita ambao anaamini watakuwa na mbinu kali wakati huu wakisaka pointi tatu kwa nguvu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali.

Alisema ni mechi muhimu sana kwao kuhakikisha wanapata pointi muhimu kwa ajili ya kusonga mbele kucheza robo fainali ya michuano hiyo kwa kuendeleza ushindi katika mechi zao hizo za makundi.

“Tunahitaji kupambana kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo miwili, ikiwamo dhidi ya AS Vita, tutakaocheza nyumbani, lengo ni kushinda na kutinga robo fainali,” alisema Gomes.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema jana jioni wachezaji wote waliokuwa na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wameungana na wenzake huku baadhi yao walikuwapo katika mataifa yao wakitarajiwa kuungana na wenzao leo isipokuwa Miquissone na Kagere.

Alisema Miquissone na Kagere wao wataripoti kambini Alhamisi kwa sababu timu zao za taifa zilikuwa na mechi jana.

“Maandalizi yanaendelea vizuri na tunatarajia hadi Alhamisi timu  imekamilika kwa wachezaji wakigeni ambao walikuwa katika majukumu ya timu ya taifa kurejea katika klabu na kuendelea kupambania timu kufikia malengo yetu ya kuhakikisha tunapata ushindi ambao utatuhakikishia kucheza robo fainali,” alisema Rweyemamu.

Kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi katika Uwanja wa Simba Mo Arena uliopo Bunju, Dar es Salaam.

Chanzo: ippmedia.com