Wikiendi iliyopita liliibuka sakata la mipira inayotakiwa kutumiwa na timu za Simba na Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, halijambo lililoifanya Yanga ipokonywe mipira ikiwa uwanjani na Simba kuazima kwa wapinzani wao.
Katika kanuni za michuano hiyo hatua ya makundi, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ndilo linatakiwa kutoa mipira maalumu ya mdhamini wao kwa timu zote zinazoshiriki na zitatakiwa kuitumia kuanzia maandalizi na hata siku ya mchezo husika.
Hata hivyo, katika michezo ya wikiendi iliyopita na ile ya ugenini, siyo Simba wala Yanga waliokuwa na mipira hiyo kutoka CAF, hali iliyowafanya waanze kuhaha kutafuta mipira huku na kule.
Ishu iko hivi, Simba kuanzia maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Raja Casablanca hapa nchini waliwaomba wageni wao mipira ya kutumia kwenye ile siku maalumu ya ‘warm up’ ambayo husimamiwa na CAF, lakini Yanga wao walilazimika kununua mipira mipya kwenye duka moja hapa jijini Dar es Salaam, lakini ikazuiwa kwanza hadi kamishna wa mchezo alipoikagua na kugundua kuwa inaruhusiwa.
Katika mchezo kati ya Yanga na Raja, Mwanaspoti lilishuhudia kamshina wa mchezo huo, Sebit Librato kutoka Afrika Kusini akimzuia Kocha wa viungo wa Yanga, Helmy Gueldich, kuendelea kupanga mipira uwanjani na kumtaka airudishe ndani. Hata hivyo, baada ya kukaguliwa alirudishiwa mipira yake na kutakiwa kuendelea na programu.
“Hapana. Kwenye kanuni za CAF Yanga walikosea kitu kidogo tu, CAF ndiyo wanatakiwa kuwapa mipira 15 kwa ajili ya michuano hii na hiyo tu ndiyo wanatakiwa kuitumia, lakini inaelezwa Yanga hawakupokea mipira hiyo kutoka CAF, siyo mara ya kwanza huwa inatokea, hivyo Yanga wakaenda kununua aina ileile ya mipira inayotakiwa dukani na kuipeleka uwanjani moja kwa moja kwa ajili ya mchezo.
“CAF hapa walichokuwa wanataka ni kama Yanga walinunua basi waipeleke kwa kamishna wa mchezo aikague na baada ya hapo atawarudishia kama inakidhi vigezo, kama haikidhi wasingetakiwa kuitumia, ndiyo maana uliona iliingizwa ndani na baada ya ukaguzi ikarudishwa kwao ikaendelea kutumika,” kilisema chanzo cha ndani.
Mbali na Yanga, pia upande wa Simba napo kulikuwa na sakata hilo hilo baada ya Simba wao kulazimika kutonunua mipira kama Yanga, lakini wakawaomba wageni wao Raja Casablanca waliowapa mipira mitano wakaitumia kwenye maandalizi ya mechi pamoja na pale uwanjani.
“CAF wanatakiwa kutoa mipira, sisi hawakutupa hadi siku ya mwisho, wapinzani wetu Raja walitupa mitano tukaitumia ile siku ya mechi, mara nyingi CAF wanaweza kuchelewa kuwapa, lakini unaweza kuiomba timu nyingine kama inayo inakupa, hili ni jambo la kawaida sana,” alisema Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu.
Hivi karibuni, Mwanaspoti liliainisha mipira inayotakiwa kutumika kwenye michuano mbalimbali ile ya Ligi Kuu Bara, michuano ya CAF na hata ile inayosimamiwa na Fifa ikiwemo Kombe la Dunia.