Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Minziro apewa "Thank You" Tz Prisons

Image 377 1140x640 Minziro Felix.png Felix Minziro

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania Prisons imeachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fredi Felix ‘Mizniro’ kufuatia matokeo yasiyoridhisha na sasa Maafande hao watabaki chini ya msaidizi, Shaban Mtupa.

Minziro alijiunga na Wajelajela hao mapema msimu huu ambapo ameiongoza mechi tisa za mashindano ya Ligi Kuu akishinda mechi moja, sare nne na kupoteza minne na kuwa nafasi ya 14 kwa pointi saba.

Hata hivyo katika mechi tisa alizosimamia Minziro ni mchezo mmoja pekee ambao hawakuruhusu bao ikiwa ni dhidi ya Singida Fountain Gate ulioisha kwa suluhu ya bila kufungana na kufanya Prisons kuwa miongoni mwa timu mbili zilizofungwa idadi kubwa ya mabao (15) ikiachwa moja na Mtibwa Sugar

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa timu hiyo umemshukuru kocha huyo kwa kipindi chote alichoitumikia huku ukieleza kuwa kwa sasa Mtupa ndiye atasimama hadi pale watakapopata wa kukabidhiwa majukumu.

Prisons inakuwa timu ya saba kuachana na kocha wake msimu huu ikiwa hata mzunguko wa kwanza haujaisha ikizifuata Simba, Namungo, Ihefu, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Singida Fountain Gate.

Simba ilimtimua kocha wake Roberto Oliveira 'Robertinho', Ihefu ikaachana na Zuberi Katwila, Coastal Union ikamtema Mwinyi Zahera, Mtibwa Sugar ikamfungashia virago Habibu Kondo huku Singida Fountain Gate ikimalizana na Mholanzi, Hans Van Pluijm na Cedick Kaze kuachana na Namungo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro amesema licha ya kusitishiwa mkataba wake lakini ameacha timu katika ari na morali na kwamba ni mapema kujua uelekeo wake akisubiri kulipwa stahiki zake.

Amekiri kuwa imekuwa mshtukizo kwake kupokea uamuzi wa mabosi wa timu kutokana na maandalizi aliyokuwa nayo kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Coastal Union, keshokutwa Alhamisi.

“Timu ilikuwa imebadilika ndani ya uwanja na nilikuwa kwenye maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi ijayo, ila kwa ujumla vijana nimewaacha kwenye ari na morali, kujua wapi naelekea ni mapema nasubiri wakamilishe stahiki zangu,” amesema Minziro.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live