Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikel Arteta awatuliza mashabiki Arsenal

Mikel Arteta Fans Mikel Arteta awatuliza mashabiki Arsenal

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewatuliza mashabiki wa klabu hiyo akiwataka watulie kwani hafikirii kuondoka kwenye kikosi hicho na yuko tayari kusaini dili jipya.

Hadi sasa mashabiki wa washika mitutu hao wa London hawaelewi hatma ya kocha wao huyo aliyewapa mafanikio katika kipindi chake akikikinoa kikosi hicho, lakini taarifa zimeibuka mazungumzo ya pande mbili yataanza mwezi ujao.

Arterta ambaye mkataba wake na Arsenal unamalizika mwakani, amewaambia mashabiki na wadau wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kwani hakuna shida yoyote licha ya kuchelewa kwake kusaini dili jipya.

Mhispania huyu anakubalika na mabosi wa juu wa Arsenal kutokana na mafanikio aliyopata katika kipindi cha miaka mitano akiiongoza hasa kwenye Ligi Kuu England ambako washika mitutu hao wamekuwa wakimaliza nafasi yapili kwa misimu miwili mfululizo.

Kwa sasa Arteta analipwa Pauni 9 milioni kwa msimu na ripoti zinadai anaweza akafikia mshahara wa Pauni 15 milioni katika dili hilo jipya.

Arteta amesema kwa sasa wapo bize na dirisha la usajili hivyo mazungumzo yataanza mara tu baada ya dirisha hili kufungwa.

"Sidhani kama kuna mtu anahitaji kuwa na wasiwasi juu ya hili, binafsi sitegemei kuondoka kwa sasa. Tupo kwenye hilo na tutalifanyia kazi kwa wakati mwafaka, akili zetu zimekuwa kwenye dirisha hili, tulikuwa na mambo mengi ya kufanya na kujadili. Nipo mahali ninapotaka kuwa na nina furaha sana, natumai viongozi nao wanafikiria kama ninavyofikiria mimi. Ninafanya kazi na wachezaji kila siku na ninapozungumza nao na kufanya majadiliano naona kwenye macho yao imani na njaa ya kupambana bado zipo.”

Katika misimu miwili mfululizo, Arsenal imekuwa moja kati ya timu tishio Ligi Kuu England ikipambana jino kwa jino na vijana wa Pep Guardiola, Manchester City.

Kutosaini mkataba mpya hadi sasa kumesababisha mashabiki wengi kuwa na wasiwasi lakini Arteta amesema:"Naona leo na kesho nitaendelea kuwa hapa."

Msimu uliopita Arsenal ilimaliza kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Man City iliyochukua ubingwa wao wa nne mfululizo wa ligi.

Arsenal ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua taji la EPL kwani ilikuwa inaongoza ligi hadi kufikia Aprili lakini mambo yakaharibika katika dakika za mwisho baada ya kuanza kuangusha pointi na kuipa nafasi Man City kuwapita na kuchukua taji.

Msimu huu Arsenal pia imeanza vizuri ligi ikishinda mechi zote mbili huku wikiendi iliyopita ikiibamiza Aston Villa mabao 2-0.

Chanzo: Mwanaspoti