Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amesifu kitendo cha ubinadamu kilichooneshwa na wachezaji wake pale walipoamua kumpa mpira mchezaji mwenzao Kai Havertz kupiga Penati kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 4-0 dhidi ya Bornemouth.
Havertz sio mpigaji wa Penati kwenye kikosi cha Arsenal lakini alipewa mpira apige na wachezaji wenzake baada ya nahodha wao, Martin Odegaard kufanyiwa madhambi na beki Christie kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo.
“Hakika nina furaha sana kwa ushindi huu, lakini nina furaha zaidi kuwa sehemu ya timu inayoonesha ubinadamu kama walivyofanya,” alisema Arteta.
“Bila ya mimi kuwaambia kufanya chochote, kuonyesha upendo kwa mchezaji ambaye watu wanahoji juu ya ubora wake, wamenifurahisha sana. Wamefanya hivyo kutoka moyoni kabisa.
“Kuonyesha ubinadamu wakiwango kile, kumjali mtu ni kitu kizuri.
“Nina furaha wamefanya uamuzi ule. Nanawashukuru mashabiki wetu kwa namna walivyoimba jina lake na kumfanya ajisikie vizuri. Kama kuna mchezaji anayestahili upendo huo basi ni Kai Havertz, nina furaha kwake.”
Kai Havertz alifunga bao lake la kwanza kwa Arsenal tangu ajiunge nao kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 65 akitokea Chelsea.
Alifunga bao hilo kwa mkwaju wa Penati baada ya Odegaard kufanyiwa madhambi na Ryan Christie.