Baada ya dirisha dogo la usajili kumalizika na kuona wachezaji mbalimbali wakisajiliwa kutoka ndani na nje ya nchi, pia tumeshuhudia baadhi wakitolewa kwa mkopo.
Baadhi ya wachezaji wametoka kwenye klabu moja kwenda nyingine. Kama inavyoeleweka kwa wanasoka kuwa mara nyingi wachezaji wanaotolewa kwa mkopo ni wale ambao wameshindwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza na cha akiba, hivyo hutolewa kwenye klabu nyingine ili wapate muda mwingi wa kucheza.
Wengine wanakuwa wameshuka viwango, hivyo wanapelekwa kwenye klabu zingine za madaraja ya kati ambazo timu zao hazina presha sana ili kurudisha viwango na kujiamini.
Wakati mwingine kuna wachezaji wana uwezo mkubwa na vipaji, lakini kwa sababu hawana majina na uzoefu wanapelekwa kwenye klabu zingine kwa ajili ya kucheza na kuthibitisha uwezo walionao, na kisha baadaye kurejeshwa tena kwenye klabu mama.
Hapa nchini, kuna wakati wachezaji wa mkopo wanakwenda 'kukiwasha' huko wanakokwenda kiasi cha klabu zao zinazowamiliki kuwarejesha tena, lakini hata hivyo wengine wakishaondoka basi hadi mikataba yao inamalizikia huko huko na wanakuwa huru, sasa inakuwa ni hiari yao kuingia mkataba na timu walikopelekwa kwa mkopo au nyingine.
Tumeona kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baadhi ya wachezaji wakipelekwa kwa mkopo sehemu mbalimbali kwa makubaliano kati ya klabu na klabu.
Hata hivyo, kumekuwa na mijadala inayoendelea kwenye majukwaa mbalimbali ya michezo kuwa wachezaji hao waachwe wacheze wanapokutana na timu zao mama.
Yaani mchezaji wa Azam FC aliyepelekwa Dodoma Jiji kwa mkopo, zitakapokutana timu hizo basi acheze tu na kusiwe na vipingamizi.
Ni kweli inawezekana kama klabu iliyomtoa haioni tatizo lolote lile, lakini isiwe nongwa kama ikikataa asicheze kwa sababu klabu mama nayo ina haki ya kufanya hivyo. Kanuni hizo zimechukuliwa kutoka Ulaya na hata walioweka hivyo walikuwa na sababu zao nzuri tu na muhimu, hivyo ziheshimiwe.
Mijadala imekuwa ikidai kuwa kitendo cha klabu mama kutomruhusu mchezaji kucheza dhidi ya timu yake iliyomtoa kwa mkopo ni kutomtendea haki mchezaji na pia klabu iliyomchukua.
Kama nilivyosema hapo juu, huu uwe ni mtazamo wa klabu yenyewe na si kuilazimisha. Ikiona acheze basi hakuna tatizo, lakini ikiona izuie na klabu iliyomchukua kukubaliana na hilo, basi makubaliano yaheshimiwe.
Nionavyo mimi ni kwamba mchezaji anayecheza kwa mkopo akicheza na kuifunga au kusababisha timu yake mama kupoteza mechi, au kutolewa kwenye michuano au kombe husika, anaweza kuwa adui kwa mashabiki na hata kama akitaka kurejea, wapenzi na mashabiki wanaweza kucharuka na kukataa.
Wengi wanaangalia upande mmoja tu kuwa mchezaji anatakiwa kuithibitishia timu yake mama kuwa ana uwezo kwa kuikamia na kucheza vizuri siku ya mechi hiyo, bila kuangalia upande wa pili kuwa anajiweka kwenye mazingira magumu pia mbele ya mashabiki.
Halafu pia kwa soka la Tanzania kuna mambo mengine ya nje ya uwanja, inawezekana kabisa mchezaji anayechezea timu kwa mkopo, akacheza chini ya kiwango dhidi ya timu yake mama kwa sababu bado ni mali yao na pia wanaendelea kumlipa mshahara. Hata kama makubaliano ya mshahara ni kila klabu kulipa nusu, lakini mkataba bado upo kwenye klabu yake ya awali.
Kwa maana hiyo, kwa maoni yangu binafsi naona kipengele cha mchezaji wa mkopo kutocheza kwenye mechi dhidi ya timu yake iliyomtoa kina afya zaidi kuliko kumruhusu kucheza.
Kinamwepusha mchezaji huyo na mengi, mbele ya mashabiki kama akisababisha timu yake mama kufungwa, lakini kutuhumiwa kucheza chini kiwango kama timu yake ya mkopo pia ikipoteza.
Kikubwa zaidi hapa ni kwamba tuziache klabu zenyewe zinazopeana mchezaji kuangalia ni vipengele gani ambavyo wanakubaliana na viheshimiwe kwa maslahi ya pande zote tatu.