Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikataba ya Aziz KI, Inonga utata Simba, Yanga

Aziz Inonga Pc Mikataba ya Aziz KI, Inonga utata Simba, Yanga

Thu, 25 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kupata nafasi ya kucheza kwa Stephane Aziz Ki na Henock Inonga kwenye timu zao za taifa za Burkina Faso na DR Congo mtawalia kunawafanya mashabiki wa Simba na Yanga kutamba hivi sasa mitaani, lakini huenda mambo ni tofauti kwa viongozi wa timu hizo.

Wakati mashabiki wakitembea vifua mbele kwamba klabu zao zina mastaa wakubwa wanaowaweka benchi nyota wanaocheza soka la kulipwa Ulaya kwenye timu za taifa, vigogo wa Simba na Yanga hivi sasa wanakuna vichwa kutokana na viwango vinavyoonyeshwa na wawili hao kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) huko Ivory Coast.

Sababu ya vigogo wa Yanga na Simba kuwa katika presha na kile kinachofanywa na Inonga na Aziz Ki kwenye Afcon ni wawili hao kutosaini mikataba mipya ambayo wamewekewa mezani na timu zao.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kuwa, licha ya Yanga kumuwekea mezani mkataba Aziz Ki, huku Simba ikifanya hivyo kwa Inonga kabla hawajaenda Ivory Coast kutumikia timu zao, bado hawajamwaga wino.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, kwa vipindi tofauti Inonga na Aziz Ki walitaka mazungumzo kwa ajili ya mikataba mipya yasifanyike sasa na badala yake klabu zisubiri hadi mwisho wa msimu, wakieleza kuwa wanataka kuelekeza akili na nguvu kuzisaidia timu za taifa na klabu kwa mechi zilizosalia za Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.

Ingawa Inonga mkataba wake umebakiza mwaka mmoja na nusu kumalizika, huku Simba inataka kumsainisha mpya ambao utamfanya abaki kwa muda mrefu.

Simba inaonekana haitaki kuingia katika presha kubwa msimu ujao ambao utakuwa wa mwisho kwa Inonga na inataka imalize biashara mapema ili kujihakikishia kubaki naye muda mrefu zaidi, ingawa beki huyo hajaonyesha dalili za kusaini mkataba mpya.

Inonga alijiunga na Simba, Agosti 2021 akitokea DC Motema Pembe na tangu hapo amekuwa mchezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo katika nafasi ya beki wa kati.

Desemba 2022, mchezaji huyo aliongeza mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili zaidi ambao utafikia tamati 2025. Hata hivyo, Simba ina mpango wa kurefusha zaidi mkataba wake kwa vile ina wasiwasi wa kupata wakati mgumu wa kupata mbadala wake katika kipindi hiki ambacho beki huyo anaonekana amezoeana vilivyo na Che Fondoh Malone ambaye anacheza naye sambamba katika nafasi ya beki wa kati.

Faida kubwa kwa Simba juu ya Inonga ni kwamba ina uwezekano wa kupata fungu kubwa la fedha ikiwa itatokea timu itakayovutiwa na kiwango kinachoonyeshwa na beki huyo katika fainali hizo zinazoendelea Ivory Coast. Kabla ya fainali hizo, tayari kulianza kuenea kwa tetesi kwamba beki huyo aliyewahi pia kutakiwa na Yanga kabla ya kuibukia Simba, alikuwa akihusishwa na dili la kwenda kucheza soka Ufaransa na Ubelgiji, japo dili hizo hazikufahamika zilifia wapi.

Tetesi za Inonga kutakiwa Ulaya zinafafa na zile ziliwahi kumtokea Pape Ousmane Sakho wakati akiwa Simba, ambapo baada ya kupuuzwa ghafla aliibukias Ufaransa ambako anaichezea timu ya Daraja la Pili iitwayo, US Quevilly-Rouen Métropole, japo hatumiki mara kwa mara kikosini.

YANGA NA AZIZ KI

Wasiwasi unaonekana kuwa mkubwa zaidi kwa Yanga ambayo mkataba wa Aziz Ki unaelekea ukingoni na bado hajasaini mpya.

Kikanuni, Aziz Ki ataruhusiwa kufanya mazungumzo na hata kusaini mkataba wa awali na klabu nyingine ikiwa mkataba wake utabakiza muda usiozidi miezi sita ufikie tamati.

Kiungo huyo amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Burkina Faso kwenye Afcon 2023 ambapo alicheza kwa dakika 86 katika mechi ya kwanza ya kundi D dhidi ya Mauritania ambayo alianza kikosini na dhidi ya Angola alicheza dakika 89, huku mchezo dhidi ya Algeria ulioisha kwa sare ya 2-2, aliishia benchi.

Hata hivyo, hivi karibuni Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alinukuliwa akitamba kuwa Aziz Ki hatoenda popote na ataendelea kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu zaidi.

“Tumeshawaambia Aziz Ki amesaini mkataba wa maisha na Yanga. Mkataba wake na Yanga ni wa maisha. Yaani jinsi sisi na Aziz Ki tunavyopendana ni leo, kesho, keshokutwa na hadi milele. Sisi na Aziz Ki mkataba wetu hauwezi kuisha,” alisema Kamwe.

Licha ya kauli hiyo ya Kamwe, lakini ukweli ni kwamba kwenye soka la kisasa hakuja mchezaji anayesajiliwa milele, hivyo lolote linaweza kutokea kwa Aziz KI iwapo watajitokeza wakataokuwa wakimhitaji.

Kwa wanaokumbuka ni kwamba, hata msimu uliopita viongozi wa Yanga walitoa taarifa kuwa ni ngumu kwa Fiston Mayele kuondoka Jangwani baada ya kuitumikia kwa mafanikio akiiwezesha kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo na Ligi Kuu Bara, lakini kilichotokea mchezaji huyo alinunuliwa na Pyramids ya Misri anakoendelea kuliamsha uwanjani.

Awali kabla ya kutimkia Pyramids, Mayele alikuwa akihitajiwa na Al Hilal ya Sudan baada ya Kocha Mkuu, Florent Ibenge aliyewahi kufanya naye kazi AS Vita ya DR Congo kumhitaji na matajiri wa klabu hiyo kuweka mkwanja wa maana, lakini wakatolewa nje kabla ya Pyramids kumbeba mwishoni mwa msimu uliopita.

Chanzo: Mwanaspoti