Kama ulidhani sakata la kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kuingia kwenye mgogoro wa kimkataba na Yanga ni jipya, sahau.
Kwenye soka la Tanzania katika miaka mitano iliyopita yametokea mambo kama hayo hasa kwa miamba ya soka nchini Simba na Yanga.
Miamba hiyo imekumbwa na migogoro ya kimkataba kwa wachezaji na watumishi wake wengine kama ilivyo kwa Fei, hata hivyo, zilimalizana nao na maisha mengine yakiendelea.
Wamepita mastaa wengi wa ndani na nje ya nchi wakakipiga kwenye timu hizo na wengine wakiacha kumbukumbu kubwa huku wengine wakiondoka kutokana na migogoro ya kimkataba na kuacha mashabiki wa timu hizo wakibaki midomo wazi wasijue nini kitafuata.
Wapo waliokuwa mihimili kwenye vikosi vyao na hivyo vigogo hao kupambana kuhakikisha wanamalizana nao fasta ili wasiwapoteze na wengine walimalizana nao na kutimkia kwengine.
Sakata kama la Kelvin Yondani, Andrew Vicent 'Dante', Ramadhan Singano ni mfano wa nyota waliotimkia kwengine kutokana na ishu za mikataba licha ya mikataba yao kufikia mwisho huku wengine wakizidai timu hizo pesa za usajili.
Mwanaspoti linakuletea matukio kama hayo lakini yaliyotikisa sana na kuacha sintofahamu kwa mashabiki na viongozi wa miamba hiyo ya soka nchini.
MORRISON V YANGA
Moja ya migogoro mikubwa ya kimkataba iliyowahi kushuhudiwa kwenye soka la Tanzania ni la winga wa sasa wa Yanga, Mghana Bernard Morrison. Sinema yake ilikuwa pigo kubwa kwa Yanga hadi kusababisha kupelekana kwenye Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya Michezo (CAS).
Ilivyokuwa: Ni misimu miwili iliyopita na alisaini Simba dirisha kubwa la usajili mwaka 2022, lakini mabosi wa Yanga akiamini bado ana mkataba nao kabla ya kwenda kumshitaki kwenye kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF na huko iliamuliwa winga huyo alikuwa huru kujiunga na Simba.
Hata hivyo, Yanga hawakuridhishwa na majibu hayo na kuamua kwenda mbele zaidi hadi CAS, lakini hata huko waligongwa mwamba na kuamuliwa kumlipa Morrison kiasi kisichopungua Sh12 milioni kama fidia na kutimiza hilo.
Morrison aliendelea kukipiga Simba kabla ya kurejea tena Yanga mwanzoni mwa msimu na kuacha sintofahamu kwa mashabiki na wengine hawakupendezwa na kurejea kwake.
CHIKWENDE V SIMBA
Katika dirisha dogo la usajili la msimu wa 2020/2021, Simba ilimsajili winga Perfect Chikwende kutoka FC Platinum ya kwao Zimbambwe baada ya kuwafunga kwenye michuano ya CAF.
Usajili wa winga huyo uliifanya Simba kumnyofoa Mkenya Francis Kahata kwenye usajili wa wachezaji wa ligi ya ndani na kubaki kimataifa kutokana na sheria za wakati huo na kuingia Chikwende.
Hata hivyo, Chikwende alishindwa kuonyesha ubora wake ndani ya Simba na vigogo wa msimbazi wakaachana naye baada ya miezi sita, lakini akawaamshia mtiti kuhusu mkataba wake ambao ulikuwa umebaki kwa mwaka mmoja na nusu.
Mwanaspoti linajua Chikwende aligoma kutolewa kwa mkopo katika timu nyingine za Ligi Kuu, pia hakwenda kwao akikaa kwa zaidi ya wiki mbili kwenye moja ya hoteli za kifahari Dar es Salaam huku Simba wakisimamia kila kitu na kumlipa baada ya kutioshiwa kupelekwa CAS.
DEJAN V SIMBA
Mletee Mzungu! ni moja ya utambulisho aliojipatia aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mserbia Dejan Georgijevic baada ya kutua kikosini hapo mwanzoni mwa msimu huu.
Hata hivyo, licha ya kujizolea umaarufu mkubwa Bongo, Dejan hakuweza kudumu Simba kutokana na matakwa ya kimkataba kutokamilika na kuamua kuondoka zake.
Miongoni mwa vitu vilivyomfanya Dejana kuondoka Simba ni kushindwa kutimiziwa matakwa yake ya kupewa nyumba nzuri kwa ajili ya familia yake, usafiri na kutopewa fedha aliyokuwa amekubaliana na mabosi hao.
Baada ya kuona matakwa yake hayatimizwi, Dejan aliikacha Simba wakati iko visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi Cup na kuondoka zake huku pande zote mbili zikipigana mkwara lakini ikaisha kimya kimya.
BIGIRIMANA V YANGA
Mwanzoni mwa msimu huu Yanga ilimsajili kiungo wa zamani wa Newcastle United ya England, Mrundi Gael Bigirimana ikiamini atalisaidia chama hilo kufikia malengo.
Gael alitua jangwani lakini hakuweza kupenya katikati ya viungo wa Yanga na mara nyingi kuishia benchi jambo lililoufanya uongozi wa timu hiyo kuachana naye mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Yanga ilimnyofoa kimya kimya Gael kwenye usajili wa ndani na nafasi yake kuingia beki mpya Mmali Mamadou Doumbia jambo lililoufanya uongozi wa Gael kutua Bongo kuidai Yanga mikwanja yake.
Hata hivyo, Yanga iliendesha jambo hilo kimya kimya na mwishowe kukubali kumlipa fidia ya kuvunja mkataba wa kiungo huyo kwa awamu pesa ambayo hadi sasa haijamaliza kumlipa.
ONYANGO V SIMBA
Mwanzoni mwa msimu huu, beki kisiki wa Simba, Joash Onyango alikuwa haonekani kikosini hapo kutokana na ishu za kimkataba.
Mwanaspoti linafahamu, Onyango alitaka kuondoka Simba baada ya kushindwa kumtimizia mahitaji yake ya kimkataba ikiwamo marekebisho ya makazi, usafiri na nyongeza ya pesa aliyokuwa akitakiwa kupewa.
Hata hivyo, baada ya Simba kusikia beki huyo akihusishwa kujiunga na watani zao Yanga, ilifanya kila kitu na kumrejesha kikosini na anacheza hadi sasa na ni chaguo la kwanza kikosini.