Wakati akisajiliwa Yanga katika dirisha dogo la usajili lililodumu kwa mwezi mmoja kuanzia Disemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, Mudathir Yahya hakuonekana kama angeweza kupenya ndani ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuachana na Azam FC pindi msimu uliopita ulipomalizika Juni, mwaka jana.
Uwepo wa nyota wa safu ya kiungo ambao walikuwa wanafanya vizuri katika kikosi cha Yanga wakati Mudathir anasajiliwa akina Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki, Yannick Bangala na Salum Abubakar 'Sure Boy' ulionekana ungekuwa kikwazo kwa kiungo huyo wa Taifa Stars kupata nafasi kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti na Mudathir ndio ameonekana kujihakikishia nafasi kikosi cha Yanga huku akiwa kipenzi cha kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi.
NGUZO LIGI KUU
Tangu alipojiunga na Yanga hadi sasa, Mudathir amecheza mechi zote tisa za Ligi Kuu ambazo timu hiyo imecheza mara nyingi akiwemo katika kikosi cha kwanza huku mara kadhaa akiingia akiwa anatokea benchi.
Katika mechi hizo tisa, Mudathir ameanza kikosi cha kwanza mara tano na ameingia kutokea benchi mara nne.
Uimara wake katika kuilinda safu ya ulinzi umeifanya Yanga iruhusu mabao sita katika mechi hizo tisa huku ikipata ushindi mara nane na kupoteza mchezo mmoja tu.
Na Mudathir hajaishia kuilinda safu ya ulinzi tu bali pia ameifungia Yanga mabao mawili ambayo yote yalikuwa ni katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji walioibuka na ushindi wamabao 4-2.
KIMATAIFA HAKAMATIKI
Mudathir amecheza mechi zote tisa za Yanga za Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia hatua ya makundi kabla ya ile ya jana ugenini ya nusu fainali dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Katika mechi hizo tisa, ameanza kikosini mara sita na kuingia kutokea benchi mara tatu huku akicheza kwa dakika 503 katika mechi hizo zote.
Na licha ya kucheza kama kiungo wa ulinzi, aemfunga bao moja katika mechi hizo tisa za Kombe la Shirikisho Afrika.
KIRAKA WA MAANA
Alitegemewa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji lakini Nabi amekuwa akimtumia pia nafasi ya kiungo mshambuliaji na matunda ya uamuzi huo yalionekana katika mchezo wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe ambao alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-1.
Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Marumo Gallants, Mudathir alikuwa anashhika nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji waliotengeneza nafasi kubwa za hatari akifanya hivyo mara nne.