Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mido Ahly aipeleka Yanga fainali CAF

Dieng Mido Ahly aipeleka Yanga fainali CAF

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Yanga ikitarajiwa kushuka uwanjani ugenini Cairo, Misri kesho Ijumaa kumalizia mechi ya makundi dhidi ya vinara wa Kundi D, Al Ahly kuna kitu kimewashtua wenyeji, baada tu ya kuona mchezo wa wageni hao walipocheza mechi ya mwisho ya nyumbani dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Ahly juzi ilikuwa ikiangalia mkanda wa mechi hiyo na kiungo mmoja wa kazi, Aliou Dieng amefichua kiwango ambacho Yanga imekionyesha iliposhinda nyumbani kwa mabao 4-0 dhidi ya Belouizdad kimewashtua na kuanza hesabu mpya.

Dieng amesema Yanga imeonyesha kiwango kikubwa katika mechi hizo tano zilizopita na kwake kama timu hiyo itakutana na timu ya kawaida kwenye robo fainali hatashangaa kuona ikicheza nusu fainali na hata kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu, kwani ina uwezo.

Kiungo huyo wa mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo na wanaotetea kwa sasa taji, amesema Yanga imekuwa na mabadiliko makubwa katika kiwango cha ubora ndani ya miaka michache ya hivi karibuni, hivyo haitashangaza kama itafika mbali zaidi kama ilivyofanya msimu uliopita ilipocheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, akisema inabebwa zaidi kwa kuwa ina wachezaji bora.

"Tulikuwa tunaangalia mechi yao iliyopita, kila mmoja akishangaa kiwango ilichokionyesha, ukikumbuka kiwango chao tulipokutana nao na hiki walichofanya kwa Belouizdad utaona hii ni timu yenye uwezo mkubwa kwa sasa," amesema Dieng na kuongeza;

"Sitashangaa kuona wanacheza nusu fainali au hata fainali kama wakikutana na timu ya kawaida kwenye hatua ya robo fainali, kitu ambacho kimewapa nguvu ni kuwa na wachezaji Bora sana ambao wamekuwa wakiamua matukio magumu uwanjani."

Pia Dieng amemtaja kipa wa taifa la Mali anakotokea yeye, Djigui Diarra kuwa ni staa muhimu kwenye ukuta wa timu yake kutokana na ubora wake wa kujua kuwapanga mabeki na hata wachezaji wengine.

"Nakutana na Djigui (Diarra) kwenye timu ya Taifa lakini nimecheza naye tangu timu za vijana kule nyumbani ni kipa mwenye uwezo mkubwa akiwa langoni namjua kwa undani sana.

"Nimekwambia Yanga ina wachezaji bora na mmoja wa hao ni Djigui, ukiwa na kipa kama huyu hakai golini kwenu akiwa kama kipa peke yake anajua sana kuwakumbusha wachezaji wote wa timu yake anaowaona mbele."

Yanga kesho itashuka Uwanja wa Kimataifa wa Cairo kuumana na Al Ahly ili kutafuta kuwa kinara wa kundi kwani zote zimeshatinga robo fainali mapema, huku zikiwa na kumbukumbu ya kushindwa kutambiana katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam kwa kufunga bao 1-1.

Kwa sasa Al Ahly inaongoza kundi ikiwa na pointi tisa, huku Yanga ikishina nafasi ya pili na nane, ikifuatiwa na Belouizdad yenye tano itakayoikaribisha Medeama iliyo na pointi nne kwenye mechi nyingine ya kufungia makundi.

Yanga imefuzu robo fainali kwa mara ya kwanza tangu CAF ilipobadilisha mfumo wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika kuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 1997 na kucheza makundi miaka 25 iliyopita kabla ya kufanya hivyo tena msimu huu na sasa inasaka heshima ya kuitinga nusu fainali kuifikia rekodi iliyowahi kuweka na Simba mwaka 1974.

Droo ya mechi za robo fainali zinatarajiwa kufanyika wiki ijayo jijini Cairo mara baada ya timu mbili za mwisho za kukamilisha Nane Bora zitakapojulikana kwani kwa sasa timu pekee zilizofuzu hatua hiyo ni TP Mazembe na Mamelodi Sundowns za Kundi A, Assec Mimosas ya Kundi B, Petro Atletico ya Kundi C na Al Aly na Yanga za Kundi D. Mechi za wikiendi hii zitatoa picha ya vinara wa makundi ya A, C na D baada ya Asec pekee hadi sasa kujihakikisha kuongoza Kundi B, lenye timu za Simba, Wydad XA na Jwaneng Galaxy.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: